SHARE

LONDON, England


NYOTA ya kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, inaonesha kuanza kufifia katika hatua ya nusu msimu tu wa Ligi Kuu ya England kuliko makocha wengine kama Jose Mourinho, Jurgen Klopp, Arsene Wenger na Mauricio Pochettino.

Wakati anatua katika ligi hiyo, wengi waliamini kuwa kocha huyo anakuja kuendeleza mafanikio yake kama alivyofanya akiwa Barcelona na Bayern Munich.

Zaidi ya hilo alitabiriwa kuwatesa makocha wengine wakubwa, lakini hadi msimu unafikia katikati matumaini yake yameanza kupungua huku wapinzani wake wakizidi kusonga mbele.

Hili linatokana na ushindani mkubwa uliopo baina ya makocha wenye CV nzuri ya soka la Ulaya ambao wameongeza mvuto wa ligi hiyo maarufu. Hii ni tathmini ya makocha sita waliopo kwenye timu kubwa za ligi hiyo, akiwemo Guardiola.

ANTONIO CONTE – ALAMA 9/10

Tunatambua mafanikio yake alipokuwa Juventus na timu ya Taifa ya Italia, lakini kasi ya mafanikio yake ya sasa nchini England yanavutia.

Ilikuwa ni bahati kwake kupewa kibarua cha kuinoa Chelsea, licha ya matatizo waliyokuwa nayo msimu uliopita na kiasi kidogo cha juhudi, ubunifu vilihitajika ili kujenga ufanisi ndani ya timu.

Mtazamo wa Conte ulikuwa kupuzia mbinu na changamoto mbalimbali ili kuwapa nafasi wachezaji wake kudhihirisha uwezo wao lakini mwanzo mzuri uliathiriwa na kupoteza mechi dhidi ya Liverpool na Arsenal.

Hatua hiyo ilimpa nafasi kocha huyo kuwataka vijana wake watekeleze anachokitaka yeye na mpango huo ukaifanya Chelsea kurudi kwenye kasi na kushinda michezo mfululizo.

Conte amejenga kikosi imara kinachojiamini akiwa na nyota kama Eden Hazard na Diego Costa, waliojenga uaminifu kwake. Chelsea inaonekana haikamatiki kwa sasa, lakini mtihani utakuja iwapo watapata majeruhi wawili au watatu katika miezi ijayo.

JOSE MOURINHO – 8/10

Licha ya Manchester United kukamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, kazi kubwa imefanywa hadi kukiimarisha kikosi hicho tangu mwanzo wa msimu.

Juhudi za makocha, David Moyes na Louis van Gaal kwa miaka kadhaa hazikuzaa matunda na yasingekuja kwa haraka kama inavyodhaniwa na wengi.

Mourinho alivyokuja kwa mara ya kwanza alionekana kuwa na matatizo kwani alihangaika mno kupata matokeo yaliyotarajiwa na mashabiki, lakini ameweza kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuchukua maamuzi magumu, likiwemo tatizo la Wayne Rooney kushuka kiwango na sasa anakimudu vyema kikosi chake kinachoridhia kufanya anachokitaka.

Bado kuna mabadiliko mengi yanayohitajika, lakini pamoja na Mourinho kuonekana anakabiliwa na changamoto kadhaa na kufurahia maisha Old Trafford, matokeo yameanza kuonekana.

MAURICIO POCHETTINO – 8/10

Ana kikosi kichanga kinachotoa upinzani kwa wapinzani wao walio Kaskazini ya London na kimeonyesha kuwa na mafanikio.

Kocha huyo ameibadili timu hiyo kwa kuunda safu ngumu ya ulinzi ambayo ilionekana nyanya.

Mashabiki watakuwa na sababu ya kuelewa kutokana na kuumia kwa miezi saba nyota wao, Harry Kane. Lakini pia uamuzi wa Pochettino kumsajili mshambuliaji, Vincent Janssen, ulikuwa wa ghafla kwani ni mchezaji ambaye atakuwa na kazi ya ziada kuonyesha ubora wake Ligi Kuu England.

Pochettino anakabiliwa na ufinyu wa bajeti ikilinganishwa na wapinzani wake na mafanikio ni jambo lililo katika mipango yake ya kila siku na hakika raia huyo wa Argentina amedhihirisha uwezo wake licha ya kukosa bahati na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Jurgen Klopp – Alama 8/10

Baada ya misimu miwili kupita, unaweza kusema Liverpool imeshiba mfumo wa Klopp na matokeo yake uwanjani yanathibitisha juhudi zake.

Wachezaji wote wanaonekana kutimiza matakwa ya kocha yanayotokana na msukumo wa mbinu zake na hakika wameimarika zaidi tofauti na msimu uliopita.

Ana wachezaji kama Philippe Coutinho na Adam Lallana wanaocheza katika kiwango cha juu na kuwafanya majogoo hao wa Liverpool kuibua upinzani mzito kwenye mbio za ubingwa.

Bado kuna pengo katika safu ya ulinzi na Klopp, anatakiwa kukabiliana na changamoto hiyo na uamuzi wake wa kumsajili kipa Loris Karius, si jibu tosha katika muda huu. Liverpool wanaonekana kuwa katika kiwango cha juu lakini safu yao ya ulinzi ni nyepesi mno pale inapokutana na timu yenye kucheza kwa presha.

Arsene Wenger – Alama 7/10

Nafasi ya nne si lengo la Arsenal kama watu wanavyodhani, bali ushindani uliopo unaifanya timu hiyo kupata wakati mgumu, ingawa bado matumaini ya mafanikio Emirates.

Usajili uliofanywa na Wenger kwa kumleta beki Shkodran Mustafi, umeifanya klabu hiyo kuwa na safu ngumu kupitika tofauti na miaka ya hivi karibuni, lakini utulivu wa kisaikolojia katika mechi kubwa bado unawawia vigumu huku ikionekana kuwa Wenger amekosa mbinu ya kukabiliana nalo.

Pep Guardiola – 5/10

Yupo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara wakiwa wamefunga mechi tatu kati ya mechi sita walizocheza hivi karibuni. Takwimu hizo haziridhishi kwa kocha ambaye anaongoza klabu tajiri katika historia ya soka Uingereza.

Matarajio ya Guardiola yalikuwa makubwa; kuipeleka Man City katika kiwango tofauti. Lakini matokeo yake hali imekuwa ngumu tofauti na ilivyotarajiwa.

Mhispania huyo alitumia gharama katika usajili wake wa majira ya joto, lakini wachezaji wachache kati yao ndio wanaofanya vizuri huku uamuzi wake wa kumtoa sadaka kipa Joe Hart na kumsajili Claudio Bravo ukionekana kumgharimu.

Safu yake ya ulinzi haina uimara lakini bado kocha huyo haoneshi jitihada za kuboresha mbinu zake huku wengine wakihisi kwamba labda anasimamia anachokiamini, lakini hiyo ni kamari mbaya anayoicheza.

Kwa gharama iliyotumika kwa kocha na wachezaji kiujumla unaweza kusema uwezo wa Man City ulioonyeshwa mpaka sasa ni wa kawaida.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here