SHARE

NA MWANDISHI WETU

MECHI iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka sio tu Tanzania mbali Afrika Mashariki na hata Afrika nzima kati ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba, dhidi ya watani zao Yanga, ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mchezo huo uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki waliyoujaza Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ulichezwa Januari 4, 2020 huku mwamuzi Jonesia Rukya akionekana kuumudu kwa dakika zote 90.

Simba ndiyo waliyokuwa wa kwanza kupata bao zikiwa zimesalia dakika tatu kipindi cha kwanza kumalizika kupitia kwa Meddie Kagere aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.

Mwamuzi Jonesia alitoa penalti hiyo baada ya Kelvin Yondani kumvuta mkono Kagere japo walilalamikia adhabu hiyo wakidai tukio hilo lilitokea nje ya boxi la penalti na Kagere akaangukia kwenye ‘kisanduku’.

Mnyrwanda huo mzaliwa wa Uganda alinyanyuka ka kuipiga penalti hiyo iliyompoteza kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo. Hili lilikuwa goli la 10 katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba walianza kwa kasi kipindi cha pili na kupata bao la pili dakika ya 47 lililofungwa na Deo Kanda kufuatia pasi nzuri ya kisigino ya Kagere iliyoanzishwa na Shomari Kapombe kwenye winga ya kulia. Licha ya kufunga bao hilo, Kanda alilazimika kutolewa nje kupata matibabu kufuatia kugongana na Adeyum Salehe.

Dakika tatu tu baada ya Simba kufunga bao la pili, Yanga walifanikiwa kupata bao la kwanza lililofungwa na Mapinduzi Balama aliyefumua shuti kali nje ya boxi la penalti lililomshinda kipa Aishi Manula na kutinga nyavuni.

Yanga walifanya shambulizi nyingine kali dakika 53 na Adeyum aliyesalijiwa dirisha dogo akitokea JKT Tanzania alimiminia krosi nzuri iliyomkuta, Mohammed ‘MO’ Banka, na kuunganisha kwa kichwa na kufunga bao lililoamsha shangwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here