SHARE

MWAMVITA MTANDA NA AYOUB HINJO

ALMANUSURA Mbeya City watibue sherehe za kuzaliwa kwa Yanga iliyotimiza miaka 85 jana baada ya kupata bao la kuongoza katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baina ya timu hizo na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Itakumbukwa Yanga ilizawaliwa mwaka 1935 ukiwa ni mwaka mmoja mbele ya mahasimu wao jadi kisoka Simba ambapo kwa mabingwa hao kihistoria jana ilikuwa ni siku ya shangwe kwa kufikisha umri huo.
Mchezo huo ulianza saa moja usiku, kwa timu zote kushambuliana na hasa Yanga wakitaka kupata bao la mapema ili kuendeleza wimbi la ushindi, lakini hata hivyo mipango hiyo haikutimia.
Kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri kwa mashabiki wa Yanga ambao walishuhudia kikosi chao kikienda mapumziko kikiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya wageni Mbeya City, likipachikwa kimiani na Lamine Moro aliyejifunga katika harakati za kuokoa mpira langoni mwake.

Bao hilo likawapa matumaini Mbeya City inayofundishwa na kocha wa zamani wa Biashara United ya mkoani Mara, Amri said.
Hata hivyo Yanga ndiyo walioanza kulisakama lango la wageni wao, wakijaribu kutengeneza nafasi mapema bila kuwa na mafanikio.

Dakika ya 11, Yanga walilisogelea lango la Mbeya City, lakini straika David Molinga hakuwa makini hivyo alishindwa kufunga bao na mpira ukapita pembeni mwa lango.

Baada ya shambulizo hilo Mbeya City, walijibu mapigo kwa Straika wao Peter Mapunda kupiga shuti kali lilogonga mwamba na kushindwa kuiandikia bao hivyo mchezo huo kuendelea kuwa wa mkali na wa kusisimua.
Burudani nyingine kwa mashabiki wa Yanga alikuwa winga wao Bernard Morrison ambaye 26 alipiga shuti la chini, lililopita pembeni kidogo mwa lango la Mbeya City.
Katika mchezo huo, kiungo wa Mbeya City, Emmanuel Memba alioneshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Morrison ambaye alikuwa akikokota mpira kuelekea lango la wageni hao.

Dakika ya 31, Mbeya City walipata bao la kuongoza baada ya beki wa Yanga, Moro kujifunga kwa kushindwa kuokoa krosi iliyopigwa na Mapunda.
Yanga walianza kwa kasi kubwa kipindi cha pili, huku wakifanya mabadiliko ya mapema kwa kumuingiza kiungo na nahodha wao Papy Tshishimbi aliyechukua nafasi ya Said Juma.
Dakika ya 49, Yanga walikosa bao kupitia kwa Molinga baada ya kushindwa kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Juma Abdul.
Straika wa Yanga, Ditram Nchimbi alioneshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya mshambuliaji wa Mbeya City, Mapunda. Ilikuwa dakika ya 60.
Mlinda mlango wa Mbeya City, Haroun Mandanda alioneshwa kadi ya njano kwa kuchelewesha muda katika dakika ya 68 ya mchezo huo.
Dakika mbili baadaye Mbeya City walifanya mabadiliko kwa kumtoa Selemani Ibrahim na nafasi yake ilichukuliwa na Samson Madeleka.
Muda wote huo Yanga walikuwa wakipambana kufa na kupona kuhakikisha wanarudisha bao hilo na dakika ya 71, walisawazisha bao hilo kupitia Morrison aliyefunga kwa kichwa kufuatia krosi safi ya Juma Abdul.
Baada ya bao hilo Yanga waliendeleza mashambulizi huku Mbeya City nao wakijaribu kulinda lango lao na kushambulia kwa kushtukiza lakini hakuna timu iliyoweza kuongeza bao.
Mchezo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, na Yanga wanasalia nafasi ya tatu wakiwa na pointi 38, wakizidiwa point 15 na vinara wa Ligi Kuu Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here