SHARE

NA WINFRIDA MTOI

MSIMU ujao, Yanga inataka kurejesha ile timu yenye kasi kutokea pembeni baada ya kusaka kifaa kingine kitakachotengeneza kombinesheni matata na Benard Morrison.

Mfumo wa Yanga wa muda mrefu, enzi za kina Simon Msuva, ni kufanya mashambulizi kwa kasi kutokea pembeni na kufanikiwa kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo.

Baada ya kuikosa ladha hiyo kwa misimu miwili mfululizo, Wanajangwani hao wamebaini winga atakayewarejeshea utamu huo ni Deo Kanda anayekipiga Simba kwasasa.

Kanda alijiunga na Simba msimu huu kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya DR Congo na mkataba wake unatarajia kumalizika mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Inadaiwa Kamati ya Ufundi ya Yanga, imeshauri kusajiliwa kwa Kanda ili kuleta uwiano mzuri katika winga kwa sababu Patrick Sibomana, ameshindwa kuziba pengo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, mazungumzo kati ya Yanga na TP Mazembe yanaendelea ili kupata saini ya nyota huyo kama (TP Mazembe) hawana mpango wa kumrejesha kikosini.

“Tayari  kamati husika imezungumza na wakala wa Kanda, pamoja na uongozi wa TP Mazembe, tunasubiri pia kwa mchezaji mwenyewe kama atakubali ofa iliyotolewa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alieleza kuwa wadhamini wao kampuni ya GSM, inasubiri kupelekewa majina ya wachezaji wote waliokubaliana na uongozi wa klabu na kujua dau ili kuanza usajili mapema.

Mkurugenzi wa Uwekezaji na Uendeshaji wa GSM, Hersi Said, aliwataka Wanayanga wasihofu na kuahidi kuwa msimu ujao watakuwa na kikosi imara kuliko timu nyingine Afrika Mashariki na Kati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here