SHARE

NA WINFRIDA MTOI

HII inaweza ikawa rekodi kwa makocha wazawa, kwani inadaiwa kuwa klabu ya Ihefu imevunja benki kwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 50 kumng’oa aliyekuwa kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila.

Katwila alijiunga na Ihefu Jumapili iliyopita muda mchache baada ya kutangaza kujiuzulu kuinoa Mtibwa Sugar aliyoanza kuitumikia tangu akiwa mchezaji.

DIMBA Jumatano lina taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Ihefu, kwamba klabu hiyo ilivunja mkataba wa kocha huyo kwa gharama kubwa ili kupata saini yake.

“Unajua Katwila alikuwa na mkataba wa miaka mitatu Mtibwa Sugar, ameitumikia kwa mwaka mmoja, hivyo ilibidi tuuvunje jambo ambalo limetufanya kutoa fedha nyingi, ni zaidi ya milioni 50,” alisema mtoa habari huyo.

Alisema, mabosi wa klabu hiyo wamefanya hivyo kwa kuamini anaweza kufanikisha malengo yao ya kuifanya Ihefu iwe moja ya timu bora Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katwila amechukua nafasi ya Makka Mwalwisi, aliyeondolewa kutokana na timu hiyo kufanya vibaya katika michezo minne ya Ligi Kuu Bara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here