SHARE

 

NA MOHAMED KASSARA

‘ITAWACHOMA sana’, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mikakati kabambe ya Yanga kusuka kikosi chao katika dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa katikati ya mwezi Desemba.

Mipango hiyo imekolezwa na Injinia Hersi Said ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni ya GSM inayoidhamini klabu hiyo, baada ya  kushare picha ya mchezaji, Anthony Akumu Agai anayekipiga katika klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Hersi kupitia ‘Insta story’ yake ameposti picha ya mchezaji huyo raia wa Kenya anayemudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji akimtakia heri ya siku yake ya kuzaliwa jana.

Picha hiyo imezua maswali mengi kuhusu bosi huyo ambaye anashilikia nyadhifa mbalimbali ndani klabu hiyo, ikiwemo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ambazo DIMBA Jumatano imezipata ni kwamba mchezaji huyo yupo katika rada za mabingwa hao kihistoria wa Ligi Kuu Bara katika dirisha dogo la usajili.

Kitendo cha kigogo huyo kumposti Akumu  kinaonyesha kuwa biashara hiyo imeshakamilika au iko katika dakika za mwisho kukamilika, huku uwepo wa Senzo Mbatha Yanga ukiongeza uhakika huo.

Senzo anayehudumu kama mshauri anatajwa kuwa sehemu ya kukamilisha dili hilo kutokana na kuifahamu vizuri Kaizer Chiefs ambayo amewahi kufanya nayo kazi siku za nyuma.

Akumu anatarajiwa kujaza nafasi moja ya mchezaji wa kigeni iliyobaki Jagwani ukiwa ni usajili wa pili baada ya hivi karibuni kuinasa huduma ya kiungo mshambuliaji raia wa Burundi, Saidi Ntibazonkiza.

Mashabiki wa Yanga wameanza kumfuatilia kiungo huyo aliyezaliwa Oktoba 20 mwaka 1992 katika mji wa Rachuonyo uliopo kwenye kaunti ya Nyanza.

Rekodi zinaonyesha Akumu ambaye pia anafahamika kama ‘Teddy’ alijiunga na Kaizer Chiefs Januari mwaka huu akitokea Zesco United ya Zambia aliyoichezea kwa miaka minne

Akiwa na jezi ya Kaizer, Akumu amefanikiwa kucheza michezo tisa na kufunga bao moja.

Akumu alianzia soka lake la kulipwa katika klabu ya Gor Mahia mwaka 2010, ambako alidumu kwa miaka minne kabla ya kutimkia Al Khartoum Al Watani Sports Club ya Sudani alipocheza kwa msimu mmoja na kurudi Kenya kukipiga na AFC Leopards kisha kumtikia Zesco United.

Hadi sasa Akumu ameichezea timu Taifa Kenya ‘Harambee Stars’ michezo 38  tangu mwaka 2011 alipoanza kuitumikia na alikuwa katika kikosi kilichocheza mchezo wa kirafiki na Zambia uliochezwa  Oktoba 9, mwaka huu na kuisadia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here