SHARE

NA JESSCA NANGAWE

MIONGONI mwa habari njema kwenye soka la Tanzania wiki hii ilikuwa ni ushindi mnono wa klabu za Simba na Mtibwa Sugar ambazo ni wawakilishi wetu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania,  Simba waliifumua bila huruma mabao 4-1 Mbabane Swallow ya Swaziland wakati Mtibwa Sugar nao wakaibutua Northern Dynamo ya Shelisheli mabao 4-0.

Utamu wa ushindi wa Mtibwa ulinogeshwa na hat trick iliyopigwa na straika wao, Jaffar Salum Kibaya, ambaye ameandika rekodi yake mpya katika maisha ya soka kimataifa.

DIMBA limemtafuta Kibaya na kufanya naye mahojiano maalumu likianzia na moto wa kucheka na nyavu alioanza nao katika Kombe la Shirikisho huku akiwa na idadi ya mabao matatu katika Ligi Kuu sawa na Kombe la Shirikisho Afrika.

DIMBA: Kwanza hongera kwa ushindi mliopata Mtibwa Sugar mbele ya Washelisheli, lakini kubwa sasa mmejipangaje mechi ya marudiano?

KIBAYA: Nashukuru sana dada yangu, tumeanza vizuri lakini bado tuna deni kubwa kwa Watanzania, tunakutana katika mchezo wa marudiano ugenini na tunahitaji kutobweteka na matokeo.

Mchezo wa soka hautabiriki wakati mwingine nasi kwakujua hilo tunakwenda ugenini akili yetu ikiwaza turudi tukiwa mashujaa.

DIMBA: Unaweza kutueleza siri ya ‘hat trick’ yako?

KIBAYA: Hakuna kingine zaidi ya juhudi zangu binafsi za mazoezi, lakini pia ushirikiano wa wachezaji wenzangu wa Mtibwa Sugar.

DIMBA: Si kwamba ile hat trick ulibahatisha?

KIBAYA: Mimi si mtu wa kubahatisha, kwangu nilitimiza jukumu muhimu langu na kwa kuonyesha najiamini nitapiga tena hat-trick mechi ya marudiano.

DIMBA: Kuelekea mechi ya marudiano wiki ijayo pengine kocha amekupa jukumu gani la ziada?

KIBAYA: Kocha ametuambia tunahitaji kupambana katika mchezo huo unaofuata ili wapinzani wetu wasije wakapindua matokeo kibabe kwani mcheza kwao hutunzwa.

DIMBA: Mnawatazamaje wapinzani wenu mechi ya marudiano?

KIBAYA: Ni timu nzuri lakini kuna vitu vingi kiufundi tunawazidi na ndio maana ilikuwa kazi nyepesi kwetu kuibuka na ushindi mnono.

Tutakwenda mechi ya marudiano tukiwa na moto ule ule wa kusaka matokeo bora ili tusonge mbele hatua inayofuata.

DIMBA: Unaitazamaje nafasi ya Mtibwa katika michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara?

KIBAYA: Tuna kikosi kipana chini ya Kocha Zubeir Katwila, ambacho kimekaa muda mrefu bila kufumuliwa, lakini tukiwa wenye nidhamu kubwa ya mazoezi na ndio maana mwenendo wetu ni mzuri.

DIMBA: Unadhani Mtibwa Sugar inaweza kutwaa ubingwa mbele ya vigogo wa soka nchini Simba, Yanga na Azam FC?

KIBAYA: Hakuna ambalo linashindikana kwetu muhimu wachezaji tukitambua majukumu yetu na tukaendeleza nidhamu tuliyonayo tunaweza kuzifyekelea mbali Simba na Yanga.

DIMBA: Huu ni msimu wako wa ngapi kwenye Ligi Kuu Bara?

KIBAYA: Msimu wangu wa nne Ligi Kuu, misimu mitatu nimecheza Mtibwa na mmoja nimecheza Kagera Sugar ambapo ilikuwa msimu uliopita kabla ya kurudi tena Manungu.

DIMBA: Dirisha dogo la usajili lipo wazi kwa sasa, upo tayari kuitema Mtibwa endapo vigogo wa soka Simba na Yanga wataweka dau nono mezani?

KIBAYA: Si Simba na Yanga tu hata Manyema FC wanaoshiriki Ligi Daraja la Tatu nipo tayari kwenda, mimi ninachoangalia  mkwanja mnono utakaovunja mkataba wangu Mtibwa Sugar. Kama kuna timu itafikia dau ninalotaka waje wachane mkataba wangu.

DIMBA: Dau lako kubwa la kwanza kusajiliwa kwenye maisha ya soka ilikuwa shilingi ngapi?

KIBAYA: Nilivuna shilingi milioni 8 wakati nasajiliwa na Mtibwa Sugar.

DIMBA: Mabeki gani Ligi Kuu unadhani kwako wamekuwa wakikupa wakati mgumu mchezoni?

KIBAYA: Hakuna mabeki wanaonipa shida labda mimi ndio nawapa shida kwa kuwa najua uwezo wangu uwanjani. Mpaka sasa nina mabao matatu kwenye Ligi Kuu na mpango wangu ni kusogea kwenye mbio za ufungaji.

DIMBA: Mipango yako ya kuendeleza soka lako zaidi ipoje?

KIBAYA: Nikiwa kama mchezaji mwenye malengo ninatamani sana kucheza soka la kulipwa kama wenzangu wanavyofanya.

DIMBA: Wewe ni shabiki wa timu gani Ulaya na mchezaji gani ni role model wako?

KIBAYA: Mimi naipenda sana Arsenal na namkubali sana Eden Hazard wa Chelsea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here