SHARE

 

James RodriguezNA NIHZRATH NTANI

SAN Jose de Cacuta ni mji mkuu wa Jimbo la Norte de Santander. Mji wa Cacuta uko Kaskazini Mashariki mwa nchi ya Colombia. Mji huu una wakazi wanaokadiriwa kufikia 650,000 kwa mujibu wa sensa ya mwisho iliyofanyika mwaka 2005.

Cacuta unashika nafasi ya sita kwa ukubwa nchini Colombia. Sifa kubwa ya mji huu ni kuwa ni wa biashara sana huku ukipakana na nchi ya Venezuela. Kwa sasa mji wa Cacuta ni maarufu sana duniani kutokana na kuelezwa ndipo mahala ambako James Rodriguez alipozaliwa.

James Rodriguez anayetajwa kuwa mmoja ya wachezaji mahiri na mwenye kipaji asilia cha soka, amezaliwa katika mji wa Cacuta, lakini amekulia katika mji mwingine wa Ibague, nchini Colombia kwa wazazi wake Willson James Rodriguez na Maria Del Pilar Rubio.

Kabla ya mwaka 2010 hakuna shabiki wa soka aliyejaribu kumfahamu Rodriguez, hadi pale FC Porto ya Ureno ilipomleta barani Ulaya kwa uhamisho wenye utata mkubwa na kugharimu fedha nyingi kutoka klabu ya Banfield ya Argentina.

Wakati Lionel Messi akiwa ana jina kubwa barani Ulaya huku akionekana wazi si chochote na si lolote nchini Argentina, Rodriguez, mtoto wa Colombia alikuwa ameliteka soka la taifa la nchi hiyo. Akiwa na miaka 17 tu tayari jina lake lilikuwa midomoni mwa mashabiki wengi wa soka nchini humo, huku pia tayari akiwa ameshathibitisha uwezo wake.

Miaka yake mitatu akiwa FC Porto ilimpelekea kutengeneza jina lake na kuzima ufalme wa Radamel Falcao klabuni hapo, ambaye aliuzwa kwenda Atletico Madrid ya Hispania. James Rodriguez alitwaa mataji matatu ya ubingwa wa Ureno na taji la Ligi ya Europa huku akitwaa tuzo mbalimbali binafsi nchini humo.

Mwaka 2013, FC Porto ilikubali Euro 45 milioni kutoka kwa klabu ya AS Monaco ya Ufaransa kwa ajili ya uhamisho wake. Ni uhamisho huo ambao kambi ya James Rodriguez ulipoweka kipengele cha kuruhusiwa kuuzwa ikiwa Real Madrid itamhitaji. Inasemekana kuwa ndoto yake ilikuwa kuichezea Real Madrid siku moja. Na hatimaye, ndoto hiyo ikaja kutimia mwaka mmoja baadaye.

Juni 5, 2014 wakati kocha wa timu ya Taifa ya Colombia, Jose Pekerman, alipotaja majina ya wachezaji 23 watakaoshiriki michuano ya fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka huo, taifa zima la Colombia lilijawa na huzuni.

Kwanini mashabiki walikuwa na huzuni? Mwanadamu mmoja aliyeitwa Radamel Falcao jina lake halikuwemo kwenye orodha hiyo ya wachezaji 23. Au kwa maneno mengine tunaweza kusema mchezaji hatari kabisa nchini Colombia na barani Ulaya kwa kipindi hicho, hakuwemo kwenye orodha hiyo.

Wakati huo ilielezwa kando ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, alikuwepo Radamel Falcao. Majeruhi yalimfanya aachwe na Pekerman na kuhitimisha kabisa soka lake. Yuko wapi Radamel Falcao ‘El Tigre’? Alikuja kama upepo na aliondoka kama upepo.

Ni katika fainali hizo za Kombe la Dunia nchini Brazil, ndipo hasa dunia ilipomfahamu James Rodriguez. Akiwa amebeba vyema majukumu ya Radamel Falcao timu ya Taifa, James alikuwa hatari kila mechi. Umahiri wake, uwezo wake wa kufunga magoli hata kuwaongoza wenzake akiwa nahodha wa timu ya taifa mdogo zaidi lilikuwa jambo la kushangaza sana. Wacolombia hawakumkumbuka tena Falcao.

Alitangaza vyema jina lake huku tukishuhudia akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo baada ya kufunga magoli sita. Pamoja na timu yake kuishia hatua ya robo fainal na kutolewa na Brazil, James alibakia kuwa shujaa wa taifa lake.

Ni baada ya fainali hiyo, James alijiunga na Real Madrid mnamo Julai 22, 2014 kwa Euro 80 milioni. Usajili huu wa James ukamfanya ashike nafasi ya nne duniani na nafasi ya tatu klabuni Real Madrid kwa wachezaji waliosajiliwa kwa fedha nyingi. Ni mahala hapo ndoto yake ikatimia.

Hata hivyo, baada ya kutumia misimu miwili  klabuni Real Madrid, James anaelekea kutolewa kafara kwa kuwekwa sokoni. Ni baada ya taifa ya Uingereza kujitoa katika jumuiya ya nchi za Ulaya. Kujitoa kwa taifa hilo kumeleta athari kubwa kwa Real Madrid. Kwa mujibu wa sheria za soka za Hispania, klabu yoyote hairuhusiwi kuwa na wachezaji zaidi ya watatu wasio raia wa nchi isiyotoka jumuiya ya Ulaya.

Kujiondoa kwa Uingereza kumepelekea kiungo, Gareth Bale, kuhesabika kuwa mchezaji kutoka nje ya jumuiya ya Ulaya. Moja kwa moja Real Madrid watakuwa na wachezaji wanne wakiwemo, Casemiro, Danilo, James Rodriguez na Gareth Bale. Hawa watahesabika kuwa hawatoki katika nchi mojawapo ya jumuiya ya Ulaya. Hali hii itapelekea mmoja kati ya wachezaji hao kuuzwa ili kubakisha watatu kama sheria inavyotaka.

Bahati nzuri ni kuwa beki wa kushoto wa klabu hiyo Marcelo na kipa Keyron Navas tayari wana uraia wa Hispania mbali na mataifa yao, baada ya kukaa nchini humo zaidi ya miaka mitano na kuomba uraia wa nchi hiyo. Hao watahesabika kuwa wanatoka Hispania.

Kwa maana hiyo Real Madrid inapaswa imuuze Casemiro, Danilo, Bale ama James lakini klabu hiyo unaonekana wazi kuwa haiwezi kumuuza Gareth Bale kwa wakati huu, huku vile vile ikiwa ni vigumu kumuweka sokoni Casemiro. Chaguo limebakia kwa beki Danilo na James Rodriguez. Huku James Rodriguez akipewa nafasi ndogo kubakia klabuni hapo kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Bila shaka James Rodriguez ndiye anayejiandaa kubeba mabegi yake na kuwahi ndege pale Barajas na kuelekea nje ya Hispania. Safari yake inaripotiwa inaweza kumfikisha Manchester United, mahala ambako amekuwa akisubiriwa kwa muda mrefu. Ni huzuni kubwa hii.

Kuondoka kwa James Rodriguez kunaweza kuleta simanzi kubwa miongoni mwa mashabiki wengi wa klabu hiyo na hata kupelekea mauzo ya jezi za klabu hiyo kushuka sokoni. James anashika nafasi ya pili kwa mauzo ya jezi klabuni Real Madrid, nyuma ya Cristiano Ronaldo.

Popote atakapokwenda James Rodriguez atakuwa ameiletea faida kubwa klabu inayomnunua, huku dau la uhamisho wake kutoka Real Madrid likitarajiwa kutopungua chini ya Euro 50 milioni. Hakika ni jambo la huzuni kwa Real Madrid itakapompoteza kiungo huyu mwenye magoli ya kusisimua na yenye kukufanya utabasamu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here