SHARE

HIVI karibuni kuliibuka mjadala juu ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kujaza idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni, ambapo inachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya timu ya Taifa Stars.
Mjadala huo ulizuka katika mitandao mbalimbali ya kijamii baada ya Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto, alipokuwa anachangia mada Bungeni mjini Dodoma kusema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ione umuhimu wa kupunguza idadi ya wachezaji hao ili kuwapa nafasi zaidi wazawa.
Mwamoto alisema kitendo cha Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuruhusu idadi hiyo kubwa ya wachezaji wa kigeni nchini ambayo ni wachezaji saba, kinawanyima wachezaji wazawa nafasi ya kutumikia klabu zao zaidi na hivyo kusababisha kurudisha nyuma maendeleo ya soka nchini na timu ya Taifa.
Kutokana na kauli hiyo, wadau wengi wa soka nchini walionyesha kutofautiana katika jambo hilo, wengine wakikubaliana na jambo hilo, huku wengine wakipinga na kusema jambo hilo si kweli.
Ukiwa kama mdau wa soka na msomaji wa ukurasa huu wa Kijiwe Utata, nini maoni yako juu ya suala hilo?

******
Mada ya wiki iliyopita
Wiki iliyopita kulikuwa na mada inayozungumzia juu ya nani kuibuka kidedea kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18?
Ligi hiyo imeanza kutimua vumbi Agosti 26 mwaka huu, katika viwanja mbalimbali nchini, huku tukishuhudia mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, Yanga, wakianza vibaya kwa kutoka suluhu na Lipuli FC ya Iringa, wakati wapinzani wao, Simba wakitoa kichapo kitakatifu cha mabao 7-0 kwa Ruvu Shooting.
Kutokana na dalili hizo za kila timu kuonekana kutoka na matokeo yake kwenye mechi za awali, wadau wengi wa soka nchini wameanza kutathmini michezo hiyo na kuanza kuhoji hatima za timu hizo.
Wachangiaji wengi walituma maoni yao juu ya suala hilo, huku kila mmoja akiamini kulingana na maono yake kuwa ni timu gani inaweza kuibuka kidedea msimu huu.

*****
Naitwa Abuu Bakari Said wa Dar, Simba ndiyo mabingwa wa msimu huu na hilo liko wazi wala halipingiki.

*****
Naitwa Muddy Mmanga wa Tanga, michuano ndiyo kwanza imeanza na bado mapema kujadili ni nani ataibuka kidedea msimu huu.

****
Mimi ni Juma Abdul wa Mwanza, Yanga watafanikiwa kutetea ubingwa wao, matokeo ya mechi za hivi karibuni yasiwakatishe tamaa wachezaji, waendelee kupambana.

****
Naitwa Samira Yusuph, Yanga ndiyo wenye kombe lao, hao Simba wasitarajie kulipata kirahisi.

*****
Naitwa Geofrey Nganja wa Tabora, msimu huu ni zamu ya Simba, wamelikosa kombe hilo kwa muda mrefu na wapinzani wao wameshaanza kupoteana, hivyo washindwe wenyewe tu.

****
Naitwa Romey Marley wa Dar, Simba ndiyo mabingwa wapya msimu huu, kombe lazima litue Msimbazi.

*****
Mimi ni Nicolas wa Arusha, nadhani Simba wanaweza kuwa mabingwa kutokana na usajili wao mzuri waliofanya na wanaonekana kujipanga zaidi.

****
Naitwa Mgembe Mgembe wa Moro, Simba hawawezi kuchukua ubingwa hata iweje, wanaanza vizuri lakini baadaye wanapoteana.

*****
Naitwa, Ngozi Jamali wa Mwanza, ni mapema mno kutabiri hilo, muhimu ni kuangalia mwenendo wa timu zote na mechi zake.

*****
Mimi ni Judith Kimario wa Dar, Ligi ndiyo kwanza imeanza na Yanga ni kawaida yao kuanza kwa kusuasua, lakini baadaye wanaonyesha makali yao.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here