SHARE

NA JESSCA NANGAWE

ULE usemi kwamba Yanga ni kubwa kuliko mchezaji, inazidi kutimia baada ya uongozi wa klabu hiyo pamoja na wadhamini wao Kampuni ya GSM, kuazimia kuzima ngebe za winga wao, Bernard Morrison, anayewasumbua.

Ishu nzima iko hivi, matajiri hao wa mtaa wa Jangwani wamejipanga kushusha nyota kutoka klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jeremy Mumbere, wakiamini ana uwezo mkubwa wa kuziba pengo hilo.

Pamoja na Morrison kutajwa kutimkia kwa watani zao Simba, Yanga haina wasiwasi baada ya kumpata mchezaji huyo.

Yanga imepanga kufanya usajili kwa umakini, ikilenga nyota wakali wa kimataifa kutokana na msimu huu kutokuwa na matokeo ya kufurahisha, ikipoteza ushiriki wa michuano ya kimataifa.

Katika toleo la DIMBA Jumapili, liliweka orodha ya wachezaji nyota watakaoshushwa na wakala wa FIFA, Maurizio Martina Tresor, ambaye ameahidi kuleta jumla ya vifaa 22 nchini   atakaowapeleka klabu mbalimbali ikiwamo Yanga.

Wachezaji hao wanaoletwa kuziba mapengo ya wachezaji wa kimatiafa wametajwa kuwa na kiwango kitakazozifanya timu za Tanzania kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

Kati ya nyota hao wanaoshushwa nchini ni pamoja na Mumbere, aliyemaliza muda wake ndani ya kikosi cha AS Vita  na ameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kumpiku Morrison.

Wakala huyo alisema, Mumbere amekuwa na mafanikio makubwa ndani ya AS Vita baada ya kucheza kwa kiwango na kuisaidia timu yake kutwaa mataji mbalimbali.

Tresor amekuwa akifanya kazi na klabu mbalimbali, akipeleka wachezaji wenye uwezo wa kufanya vizuri kimataifa, hususan kwa timu maarufu za Afrika.

Kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela, wapo katika  harakati za kuboresha kikosi chao, lakini  kuweka wazi mipango yao ya usajili ni hadi kikosi chao kitakapomaliza mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizosalia.

Alisema hawana haraka yoyote ya kufanya usajili, lakini tayari wana majina ya wachezaji waliyoanza nao mazungumzo wakiwemo watano wa kigeni na wanne kutoka hapa nyumbani.

“Suala la usajili kwetu halina haraka, tupo na mipango imara ya kurejesha furaha ya mashabiki, tunajuwa wameumizwa na matokeo ya timu yetu kwa msimu huu lakini tunajipanga kikamilifu, hatutaki haraka katika jambo kubwa la usajili lenye maslahi mapana kwa klabu,” alisema Mwakalebela.

Yanga inakabiliana na mechi mbili zote ugenini ili kuhitimisha michuano ya Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo leo wanavaana na Mtibwa Sugar mjini Morogoro kabla ya kusafiri kwenda Iringa kucheza na Lipuli FC, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Samora Jumapili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here