SHARE

NA CLARA ALPHONCE


 

AZAM wanayo jeuri ya fedha, asikwambie mtu kwani wameamua kurudi Simba na kuwaambia wanamtaka mchezaji wao wa zamani, John Bocco, kwa gharama yoyote ile.

Taarifa za uhakika ambazo DIMBA Jumatano imezinasa kutoka pande zote, zinadai kuwa Azam walikwenda kuomba kumrejesha kundini Bocco, kwa madai kuwa walifanya kosa kubwa kumuuza kwani yeye ni kama nembo ya Wanalambalamba hao.

Taarifa hizo zinadai kuwa timu hizo zilifanya mazungumzo marefu na Simba wakawaambia wenzao waweke mezani kitita cha Sh milioni 100, lakini Azam wakasema wao watapandisha mpaka Sh milioni 150 kwa jinsi wanavyoihitaji huduma ya straika huyo.

“Jamaa wanamhitaji sana Bocco, wametuambia yeye ni kama alama ya Azam FC na walimtoa kimakosa na tukawaambia waweke mezani Sh milioni 100, wao wakasema wataleta Sh milioni 150 kabisa,” alisema kigogo mmoja wa Simba.

Hata hivyo, baada ya taarifa hizo kuvuja, DIMBA Jumatano lilimpigia Mwenyekiti wa Azam FC, Nassor Idrisa ambaye hakukiri kuhusu suala hilo zaidi ya kusema wanaheshimu mkataba alionao Bocco ndani ya Simba.

“Jonh Bocco ni mchezaji mzuri na kila timu ingependa kuwa naye lakini hizo taarifa za kuwa tunataka kumrejesha, hazina ukweli, sisi tunaheshimu mkataba alionao pale Simba.

“Azam FC ikifika wakati wa usajili yanaibuka mambo mengi, hapa kuna taarifa kuwa tumempigia simu beki wa Yanga, Kelvin Yondan, tunamtaka Shiza Kichuya wa Simba, vitu ambavyo si vya kweli, kama hivyo Azam FC itasajili wachezaji wote basi,” alisema Nassor.

Hata hivyo, licha ya mwenyekiti huyo kukanusha, taarifa nyingine zinadai kuwa vigogo wazito ndani ya Wanalambalamba hao ndio waliokaa na kukubaliana kufanya kila linalowezekana kumrejesha Bocco.

Kwa upande wao, Simba licha ya mmoja wa viongozi hao kusema wapo tayari kumwachia Bocco, viongozi wengine wamesema jambo hilo halitawezekana kabisa kutokana na umuhimu wake ndani ya kikosi hicho.

“Tutakuwa watu wa ajabu sana kama tutamwachia Bocco, unajua sisi tunajipanga na michuano ya kimataifa msimu ujao halafu tuuze mfungaji makini kama huyo, hiyo haitawezekana,” alisema kigogo mmoja wa Simba.

Kwa upande wake, Kaimu Rais wa Klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try again,’ alisema masuala yote yanayohusu usajili aulizwe Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zacharia Hanspoppe ambaye hata hivyo hakupatikana kwenye simu yake.

DIMBA Jumatano lilipomtafuta Bocco mwenyewe, alisema kwa kifupi: “Hayo ni masuala binafsi, ninachoweza kukwambia mimi bado ninauheshimu mkataba wangu na Simba na sasa akili yangu ipo kuhakikisha tunaipatia timu ubingwa, hayo mengine siwezi kuyazungumza.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here