SHARE

MWAMVITA MTANDA

STRAIKA hatari wa Wekundu wa Msimbazi (Simba), Meddie Kagere, jana alirudisha tabasamu kwa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitokea nchini Rwanda.

Kagere pamoja na wachezaji wengine walitawanyika baada ya michuano ya Ligi Kuu Bara kusimamishwa Machi 17 mwaka huu kufuatia kuzuka kwa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona na hivyo Serikali kuzuia matukio yote yanayosababisha mikusanyiko ya watu.

Kwa kipindi hicho, Kagere alikuwa Rwanda akiendelea kujifua huku mara kadhaa akiposti mitandaoni jinsi alivyokuwa akijiweka sawa tayari kukabiliana na michuano ya ligi itakaporuhusiwa.

Hatimaye kinara huyo wa kupachika mabao ndani ya kikosi chake pamoja Ligi Kuu Bara kwa ujumla alipata taarifa kwamba michezo hiyo inatarajia kuanza Juni Mosi maka huu baada ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, kuiruhusu kuanza kutimua vumbi.

Kagere akifuatana na kocha wa timu ya Namungo FC, Hitimana Thierry ambaye naye alikuwepo nchini Rwanda, waliwasili katika uwanja mdogo wa Ndege Dar esSalaam wakitokea jijini Mwanza, ambako ndiko walikounganisha safari ya kutoka jijini Kigali.

Akizungumza baada ya kuwasili uwanjani hapo, Kagere aliyekwisha pachika mabao 19 Ligi Kuu Bara, alisema amekuja kujiunga na wenzake kwa ajili ya kutetea ubingwa wao. Alisema, yeye pamoja na wachezaji wenzake wa Simba, waliumizwa na kitendo cha ligi kusimama kwa vile walikuwa katika hatua nzuri ya kutetea ubingwa wao.

Hata hivyo anaamini kukutana tena na wenzake kutawaongezea mzuka wa kufanya vizuri uwanjani ili kutimiza malengo ya timu ya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.

Hadi michuano hiyo inasitishwa tayari Simba ilishakuwa kileleni ikiwa na jumla ya pointi 71 baada ya kucheza mechi 28.

Nafasi hiyo inaipa matarajio makubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na tofauti kubwa ya pointi na timu mbili zilizopo chini yake, ambapo Azam FC inashika nafasi ya pili kwa pointi 54 ambazo ni pungufu ya 17 huku Yanga yenye pointi 50 itahitaji kuongeza 21 ili iwe sawa na mabingwa hao watetezi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here