SHARE

NA WINFRIDA MTOI

LAZIMA wakae. Ni kauli ya Wanayanga wengi baada ya kocha wao, Cedric Kaze, kusema mashabiki wa timu hiyo kesho wataanza kufurahi ubora wa kikosi chao baada ya kuingiza fomesheni mpya kwa ajili ya kuipigisha kwata Polisi Tanzania.

Yanga inatarajia kukutana na Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kutokana na kauli za kocha huyo na mazoezi aliyofanya tangu Jumamosi wiki iliyopita akiwa na kikosi hicho, mchezo na Polisi Tanzania, itashuhudiwa Yanga yenye vitu tofauti.

Msimu uliopita kutokana na udhaifu wa kikosi hicho katika baadhi ya maeneo, iliifanya Yanga ishindwe kutamba mbele ya maafande hao kuambulia sare nyumbani na ugenini.

Licha ya msimu huu kuanza vizuri bila kupoteza mechi, bado hamu kubwa ya Wanajangwani hao ni kuona kikosi chao kinacheza soka la kuvutia.

Kilio hicho ni kama Kaze alikisikia kabla ya kujiunga na timu, kwani ameahidi kubadilisha aina ya uchezaji kwa kuja na mifumo mbalimbali ya kuifanya Yanga kuwa na kasi zaidi uwanjani na kucheza soka la burudani na kupachika mabao.

Kuanzia kesho katika mchezo na Polisi Tanzania, fomesheni ya Kaze ni kuhakikisha timu hiyo inapata mabao na inacheza mchezo wa kuwanyima wapinzani nafasi na kuwapa presha.

Akizungumzia mchezo huo, Kaze alisema utakuwa ni mzuri na anatarajia kuona ushindani kutokana na alivyofuatilia mechi za Ligi Kuu Bara.

Kaze alisema katika siku chache alizokaa na wachezaji anajaribu kufanya kile kinachowezekana kwa michezo iliyopo mbele yao, hususan kuwaweka fiti nyota wake.

“Jambo muhimu kwanza ni wachezaji kuwa fiti na kuweza kucheza dakika 90 bila shida, kuelekea mchezo wetu na Polisi Tanzania, tumejipanga vizuri, Wanayanga watarajie mazuri.

“Tunashukuru tumeanza vizuri, vijana wanajitoa kwa moyo mmoja, kikosi kipo katika hali nzuri, lakini tutawakosa wachezaji watatu,” alisema Kaze.

Aliwataja wachezaji hao kuwa Carlos Carlinhos anayeumwa, Abdulazizi Makame na Mapinduzi Balama ambao ni majeruhi.

Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Simon Patrick, ameliambia DIMBA Jumatano kuwa kuna uhakika wa kocha huyo kukaa katika benchi kesho kutokana na vibali vyake kukamilika.

“Hapa tunapozungumza (jana), nipo nashughulikia vibali vya mwalimu, maendeleo ni mazuri, Alhamisi atakuwepo katika benchi kwa sababu sehemu kubwa tumemaliza,” alisema Patrick.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here