SHARE

MADRID, Hispania


TAA nyekundu imewashwa. Hatari inaweza kutokea muda wowote kuanzia sasa, baada ya kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois kuwapiga mkwara mzito wapinzani wao katika Ligi Kuu Hispania, La Liga, na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kipa huyo wa zamani wa Chelsea anaamini kikosi chao cha Real Madrid kitakuwa moto wa kuotea mbali zaidi msimu ujao baada ya kushinda taji la La Liga msimu huu.

Hata hivyo, Courtois amewaambia mashabiki wa Real Madrid kuwa staa wao mpya, Eden Hazard ndiyo atafanikisha kuiongoza timu hiyo kuelekea katika mafanikio hasa ya kushinda taji la La Liga kwa mara nyingine.

Itakumbukwa Hazard hajaonyesha kiwango kizuri tangu alipojiunga na Real Madrid akitokea Chelsea kwa kitita cha pauni milioni 100.

Lakini Courtois anaamini huu ni wakati sahihi wa staa mwenzake wa timu ya Taifa ya Ubelgiji kuanza kuonyesha kiwango bora tangu alipoingia Santiago Bernabeu.

“Hazard yuko vizuri, si mchezaji ambaye anahitajika kuelezewa sana sababu ya kile alichokifanya England, lakini alikuwa na wakati mbaya mwanzoni mwa msimu hapa.

“Mambo anayofanya sasa kila mtu anashangaa, wote tunaamini atakuwa msaada mkubwa kuelekea msimu ujao wa La Liga ikiwezekana kushinda taji hilo kwa mara nyingine.

“Anahitaji muda kuonyesha kiwango chake, lakini ni mchezaji mkubwa ambaye amekuwa akiwashangaza wengi anapokuwa na mpira hata mazoezini, ni ngumu kumzuia.

“Kama akiendelea kuwa hivi, basi uhakika utakuwa mkubwa wa kushinda hata taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu au ujao, ni mchezaji wa daraja la juu ambaye anastahili kuvaa jezi ya Real Madrid,” alisema.

Hazard alilalamikiwa na mashabiki wa Real Madrid kwa kushindwa kufanya vizuri ndani ya kikosi hicho, katika kipindi cha miezi sita kabla ya ligi kusimama alicheza michezo miwili tu.

Kabla ya La Liga kusimama, Real Madrid walizidiwa pointi mbili na Barcelona katika msimamo wa Ligi Kuu, lakini walifanikiwa kupindua meza na kutwaa taji hilo msimu huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here