SHARE

NA MOHAMED KASSARA

HALI siyo shwari ndani ya klabu ya Simba baada ya jana uongozi kuitisha kikao na kufanya uamuzi mgumu wa kutimua baadhi ya viongozi na pia kutoa onyo kwa wengine waliobaki.

Waliokumbwa na panga hilo, ni pamoja na Meneja wa Timu, Patrick Rweymamu, kocha wa makipa, Mohamed Mwarami, na mfanyakazi mmoja katika kitengo cha mawasiliano aliyefahamika kwa jina la Ally Shatry maarufu kama Chico.

Habari ambazo DIMBA Jumatano limezipata zimesema, viongozi hao wameondolewa kutokana na kutowajibika vizuri na hivyo kupelekea timu kufanya vibaya.

Taarifa hizo zimesema kuwa, makosa yaliyosababisha kocha Mwarami kutimuliwa ni kutokana na udhaifu alioonyesha kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula, katika mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons uliomalizika kwa kukubali kichapo cha bao 1-0.

Katika mchezo huo Manula alifungwa bao la mbali, huku kipa namba mbili Beno Kakolanya, naye akionyesha udhaifu wa kutema mikwaju mingi na pia kuachia bao katika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting, iliyochezwa juzi na mabingwa hao watetezi kupoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Katika hatua nyingine, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Simba, Barbara Gonzalez, ameitisha kikao kizito na benchi la ufundi la timu hiyo akitaka kujua nini chanzo cha matokeo mabovu hususan katika mechi mbili za ligi.

Wekundu hao Msimbazi wamejikuta wakikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ruvu Shooting mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ikiwa ni siku nne tu baada ya kufungwa bao 1-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Matokeo hayo yamechafua hali ya hewa ndani klabu hiyo, huku mashabiki nao wakishindwa kufumbia macho mwenendo wa kikosi chao, kidole cha lawama kikielekezwa kwa kocha mkuu, Sven Vandenbroeck.

Baadhi ya wadau wamedai kukosekana kwa wachezaji wao muhimu kama Meddie Kagere, Clatous Chama na Chris Mugalu ndiyo sababu iliyoifanya timu hiyo kushindwa kupata ushindi katika michezo hizo.

Licha ya kukosekana na kwa Kagere na Mugalu ambao ni majeruhi, Sven alianza bila mshambuliaji asili wa kati katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, huku akimuweka nje Charles Ilanfya na John Bocco akiingia kutokea benchi.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ambazo DIMBA Jumatano imezinasa ni kwamba, CEO huyo amemtaka kocha Sven ajieleze kipi kinaisibu timu hiyo.

Barbara amemuweka kitimoto Sven baada ya kutilia shaka mwenendo wa kikosi hicho kuelekea mchezo dhidi ya watani zao, Yanga, utakaochezwa Novemba 7, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Licha ya mechi hiyo ya watani wa jadi, Simba inakabiliwa na michuano ya kimataifa inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi ujao, hivyo mwenendo huo mbovu umeushitua uongozi na kuamua kuitisha kikao hicho.

Sven ametakiwa kutoa maelezo ya kina kwanini timu hiyo inashindwa kupata ushindi baada ya kuwakosa baadhi ya nyota wake ukizingatia timu hiyo ilifanya usajili wa nguvu ili kujenga kikosi imara.

Kocha huyo anashutumiwa kwa kutokuwa na maelewano mazuri na wenzake katika benchi la ufundi, hapendi kushauriwa na pia amekuwa akiwatenga baadhi ya wachezaji.

Ikumbukwe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (MO) wakati akizungumza na wahariri wa habari za michezo hivi karibuni katika hoteli ya Hyatt, alikiri wazi kuwa kocha huyo amekuwa na msimamo wa kutopenda kushauriwa.

“Katika makocha wenye misimamo yao tuliopata ni huyu, hapendi ushauri na kila kitu anataka kuachiwa yeye mwenye, sisi kama viongozi tumemuachia kila kitu,” alisema MO.

Licha ya vichapo hivyo mfululizo, Simba bado ipo nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na jumla ya pointi 13 katika michezo saba iliyokwishacheza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here