SHARE

NA WINFRIDA MTOI

HALI ya maambukizi ya virusi vya Corona imezidi kuleta sura tofauti katika tasnia ya michezo baada ya Yanga nao kuja na mbinu mpya ya kufanya mazoezi.

Baada ya Wizara ya Afya nchini kutangaza kuwepo kwa mgojwa mmoja aliyepata maambukizi hayo, uongozi wa klabu hiyo umeshutuka na kutengeneza utaratibu wa kuwakinga wachezaji wake.

Utaratibu ambao Wanajangwani hao wamekuja nao ni kuwazuia mashabiki na watu wengine wasiohusika na mazoezi kuingia kwenye uwanja wanaotumia kujifua ikiwemo pia kambini.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Yanga, Hassan Bumbuli, alisema watakuwa wakiwasiliana na madaktari kila mara kujua utaratibu mzuri wa kufanya mazoezi.

Bumbuli alisema mkakati wa kwanza uliopitishwa na uongozi ni kuzuia watu mazoezini wakiwamo waandishi wa habari.

“Tulikuwa na utamaduni wa kuwaruhusu watu mbalimbali wanaotaka kuona mazoezi kufika uwanjani, lakini kuanzia kesho (leo) litakuwa ni benchi la ufundi na wachezaji pekee.

“Tunataka kuwaweka wachezaji wetu katika hali ya usalama, hili tatizo la virusi vya Corona limekuwa kubwa na tayari Tanzania ametangazwa mgojwa,” alisema Bumbuli. Alisema kikosi hicho baada ya kurejea kutoka Lindi, wachezaji walipewa mapumziko ya siku mbili, sasa kazi inaanza ya maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu Bara ambayo hata hivyo imeahirishwa kwa muda wa mwezi mmoja kufuatia agizo la Serikali kusitisha shughuli zozote za michezo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here