SHARE

 

LONDON, England


 

KWA mashabiki wa kandanda, leo ndiyo siku ya Atletico Madrid na Maresille kuvaana katika mtanange wa fainali ya Ligi ya Europa ambao unatarajiwa kuchezwa mjini Lyon, Ufaransa.

Vijana wa Diego Simeone walitinga fainali kwa kuiondoa Arsenal, huku wapinzani wao, Marseille, wakiwasukuma nje RB Salzburg ya Australia.

Huo utakuwa ni mchezo wa tatu kuzikutanisha timu hizo baada ya kuvaana katika mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (2008-09), ambapo Atletico walishinda mechi ya kwanza, kabla ya kutoa sare mchezo uliofuata.

Marseille wanatarajiwa kushuka dimbani bila nyota wake, Rolando, ambaye bado anauguza majeraha, lakini Atletico wanachekelea kurejea kwa nyota wake, Filipe Luis.

Lakini sasa, wakati wengi wakiusubiri mchezo huo, kuna vita kali kati ya Antoine Griezmann atakayekuwa na kikosi cha Atletico na Florian Thauvin wa Marseille.

Nyota hao ambao ni raia wa Ufaransa, msimu huu wamekuwa moto wa kuotea mbali mbele ya walinda mlango na wanatarajiwa kuwa kivutio kikubwa katika mchezo huo utakaochezwa mjini Lyon, Ufaransa.

Thauvin ameziona nyavu mara 26 na kutoa ‘asisti’ 17  msimu huu, akimzidi mpinzani wake, Griezmann ambaye amefunga mabao 27 na kutoa pasi za mabao 13.

Wakati huo huo, Thauvin mwenye umri wa miaka 25, ameweza pia kuwafunika mastaa wanaotajwa kuwa na majina makubwa Ligue 1 msimu huu, Kylian Mbappe (mabao 21, asisti 16), Dimitri Payet (mabao 10, asisti 22) na Nabil Fekir (mabao 23 na asisti nane).

“Kikosi chetu kina sifa zote za kushinda. Tunachokifikiria sasa ni ushindi tu,” alisema kiungo wa Atletico, Gabi.

Kwa upande wake, staa wa Marseille raia wa Ureno, Rolando, alisema: “Tangu kuanza kwa msimu huu, kocha (Rudi) Garcia amekuwa akisema kuwa hatutakuwa na kizuizi.”

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha kwanza cha Marseille kinatarajiwa kuwa hivi: Mandanda; Sarr, Rami, Luiz Gustavo, Amavi; Sanson, Lopez ; Thauvin, Payet, Ocampos na Germain.

Kwa upandwa wake, ‘first elcven’ ya Atletico huenda ikawa hivi: Oblak; Vrsaljko, Savic, Godin, Lucas; Koke, Saul Niguez, Gabi, Correa; Griezmann na Costa.

 

*****

Mancini amrejesha Balotelli kikosini

MILAN, Italia

KOCHA Roberto Mancini ambaye atakuwa na timu ya Taifa ya Italia, amesema milango iko wazi kwa Mario Balotelli kurejea kikosini.

Mancini aliyasema hayo katika mahojiano yake ya kwanza na waandishi wa habari baada ya kutajwa kuwa ndiye atakayeiongoza Italia iliyoshindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.

Baada ya kupewa kibarua hicho, gumzo kubwa lilikuwa ni hatima ya Balotoelli kwa kuwa alikaribia kuzichapa na Mancini wakati walipokuwa Manchester City.

“…Italia inahitaji wachezaji wa kiwango cha juu. Nitazungumza na Balotelli,” alisema Mancini na kuongeza: “Umri ni muhimu kwa sababu tunataka kuwa na kesho yetu,” alisema Mancini.

Baada ya kushindwa kung’ara England akiwa na Liverpool, Balotelli mwenye umri wa miaka 27, amekuwa hatari akiwa Nice, ambako amepachika mabao 43 kwa misimu yake miwili Ligi Kuu Ufaransa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here