SHARE

NA SAADA SALIM

SIRI imefichuka!
Hivi unajua kwamba Straika wa Stand United, Alex Kitenge, Jumapili iliyopita wakati timu yake ilipoivaa Simba katika mchezo wa Ligi uliopigwa Uwanja wa Taifa, hakuwa fiti kiafya? lakini alilazimika kucheza hivyohivyo, huku akiwa na malengo yake kichwani.
Kitenge, raia wa DR Congo, anayeishi Burundi, kwa sasa ndiye aliyeweka rekodi ya kufunga hat trick katika michuano ya Ligi Kuu akifunga mabao hayo wakati timu yake ilipoicheza na Yanga.
Kufuatia uwezo anaoendelea kuuonyesha, tayari jina lake limekuwa likitajwa na klabu kubwa nchini, ikiwemo Simba, katika kipindi hiki cha kuelekea usajili wa dirisha dogo.
Baada ya kuzipata taarifa hizo, Kitenge aliona ipo haja ya kuwanyoosha Simba katika mchezo huo ili kudhihirisha ubora wake, lakini tofauti na dhamira yake akajikuta timu yake ikipoteza mchezo huo kwa kufungwa 3-0.
Habari za Wanamsimbazi kuiwinda saini ya Straika huyo zimeanza kusambaa, ingawa Kocha Mkuu, Patrick Aussems, alipoulizwa na Dimba Jumatano, hakutaka kuzungumzia hilo na kudai kwa sasa kikosi chake kipo katika mikakati ya kufanya vizuri kwenye ligi na michuano ya Kimataifa.
Hata hivyo, Kitenge mwenyewe alisema amekuwa akipata wakati mgumu sana katika ligi kutokana na mabeki wa timu pinzani kumkamia zaidi, ila atahakikisha anapambana kuendelea kufunga ili kujiweka katika mazingira mazuri yatakayowavutia viongozi wa timu kubwa.
Alisema anahitaji kufanya vizuri ili kupata nafasi katika timu nyingine, huku akiitaja Simba kwamba ni timu ambayo anatamani kucheza nayo, hasa katika duru la pili la ligi hiyo.
“Simba ipo vizuri ukiangalia, inacheza kwa mipango, natamani sana kucheza ndani ya kikosi cha timu hiyo, kwani nina imani nitaenda kukutana na Meddie Kagere, ambaye niliwahi kucheza naye tukiwa Kenya,” alisema Kitenge.
Simba kwa sasa ina kikosi kipana, hasa safu ya ushambuliaji, ambapo imekuwa ikiwatumia sana Emmanuel Okwi, Kegere, John Bocco, Adam Salamba na Shiza Kichuya, huku mastraika wengine wakipangwa katika mechi chache.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here