SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

KATI ya michezo ya Ligi Kuu mbalimbali barani Ulaya iliyopigwa mwishoni mwa wiki, gumzo kubwa lilikuwa ni timu ya Barcelona kujizolea ushindi wa kishindo wa mabao 5-0 dhidi ya Sporting Gijon bila huduma ya mshambuliaji wake tegemeo kikosini, Lionel Messi, huku kwa mahasimu wao Real Madrid, wakilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Las Palmas.

Katika mechi ambayo Madrid walikuwa ugenini kwenye dimba la Estadio de Gran Canaria, Kocha wa Madrid, Zinedine Zidane, alilazimika kumtoa supastaa wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo, ambaye alibanwa vilivyo kiasi cha kushindwa kufunga bao lolote.

Kwenye Ligi ya Kuu ya Italia, maarufu ‘Serie A,’ mlinda mlango namba moja wa timu ya taifa ya England anayekipiga katika klabu ya Torino kwa mkopo akitokea Manchester City, Joe Hart, alifanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza katika klabu yake hiyo mpya.

Kwa upande wa Ligi Kuu England, hatimaye mchezaji wa bei ghali duniani, Paul Pogba, alifanikiwa kufunga mjadala kwa muda kutoka kwa mashabiki waliokuwa wakiukosoa uwezo wake baada ya kuingia kimiani katika ushindi mabao 4-1 dhidi ya Mabingwa watetezi, Leicester City, huku pia akiibuka nyota wa mchezo huo uliopigwa katika dimba la Old Trafford.

Lakini pia katika ligi hiyo pendwa inayotazamwa na idadi kubwa ya mashabiki ulimwenguni kote, tukio hilo la Pogba kuanza kuonyesha umahiri, lilionekana kuvuta hisia za wengi.

Katika ligi hiyo, jumla ya timu 17 kati ya 20 zimeshuka dimbani mara sita, isipokuwa kwa timu za Watford, Burnley na West Ham ambazo zina michezo mitano kila mmoja.

Manchester City ya kocha Pep Guadiola, wenye pointi zao 18 wanaongoza ligi hiyo wakiwa wameshinda michezo yao yote, huku mkiani Sunderland ya David Moyes ikibeba timu zote 20, hadi sasa akiwa ameambulia pointi moja pekee.

Ligi hiyo inao makocha wenye rekodi ya juu katika soka kama kina Jose Mourinho (Manchester United), Antonio Conte (Chelsea) na Jürgen Klopp (Liverpool) ambao kwenye vikosi vyao kuna mastaa kama Eric Bailly, Zlatan Ibrahimovic, Kun Aguero, Oscar na Adam Lallana.

Lakini pia wako mafundi wengi wa soka, hususan eneo la kiungo, walionunuliwa kwa ‘bei mbaya’ kutokana na usajili wao kuwa wa bei ghali, kama akina Paul Pogba wa Manchester United na wengine ambao wanapokea mishahara minono kila wiki kama ilivyo kwa nyota matata wa Manchester City hivi sasa, Kevin De Bruyne, pamoja na kina Roberto Fermino, Riyad Mahrez, Dimitri Payet na Mesut Özil.

Licha ya wakali hao kuziongoza timu zao kuibuka na ushindi mnono mwishoni mwa wiki iliyopita na kuziweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, lakini wamejikuta wakipigwa bao na kiungo wa bei chee wa Crystal Palace, Jason Puncheon, mwenye thamani ya pauni milioni 2, ambaye aliibuka kinara kwa takwimu kwa upande wa kutengeneza pasi sahihi.

Puncheon, raia wa England mwenye umri wa miaka 30 aliyesajiliwa na Crystal Palace akitokea Southampton hadi sasa, katika michezo sita iliyopita akiichezea timu yake hiyo mpya amewafunika viungo matata wa timu kubwa na wa bei mbaya kama kina Pogba, kutokana na kutengeneza pasi 22 murua kwa timu yake ya Crystal Palace, ambayo ilipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Sunderland Jumamosi.

Katika mchezo huo uliopigwa dimba la Light, Puncheon alitengeneza nafasi 8 kwenda kwa washambuliaji Ledley, McArthur na Christian Benteke na kuwagaragaza Kevin De Bruyne (Manchester City), Willian (Chelsea) na Roberto Fermino (Liverpool), Riyad Mahrez (Leicester City), Dimitri Payet (West Ham) na Mesut Ozil (Arsenal).

Puncheon, licha ya kutengeneza nafasi 22, pia aliweza kutoa pasi za mwisho mbili, vilevile akiwa na asilimia nzuri 85.3 katika kupiga pasi sahihi kwenda kwa mlengwa.

Baada ya mchezo huo kumalizika kiungo huyo alimwagiwa sifa na kocha wake Alan Pardew kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha wa kuunganisha timu.

“Puncheon amekuwa muhimili mkubwa ndani ya timu. ‘Movement’ zake ni za uhakika kabisa na hata anachokifanya kinasisimua.
“Kizuri zaidi ni upigaji wake wa pasi ambazo asilimia kubwa zimekuwa sahihi na za kuisaidia kumfanya mpinzani kutaabika. Ni kitu kizuri kuwa na mchezaji wa aina hii,” alisema.

Ingawa ameonyesha uhodari mkubwa katika suala zima la kutengeneza nafasi, tangu msimu uliopita lakini safu ya ushambualiaji iliyokuwa ikiongozwa na Marouane Chamakh na Emmanuel Adebayor, ilionekana kumuangusha kutokana na kutotumia vema pasi hizo na kupelekea Pardew kuchukizwa na hilo, lakini moto wake hivi sasa umekuwa maradufu na wenye manufaa.

Hata hivyo, kutokana na ubutu wa mastraika hao, ilibidi kocha huyo kumsajili straika wa kiwango cha juu msimu huu, Christian Benteke kutoka Liverpool kwa pauni milioni 27, pamoja na Loic Remy kutoka Chelsea kwa mkopo wa muda mrefu.

Orodha ya nyota waliotengeneza pasi nyingi msimu huu ndani ya mechi sita walizocheza katika vikosi vyao kwenye Ligi Kuu England ni kama ifuatavyo:
1. Jason Puncheon, 22
2. Kevin De Bruyne, 20
3. Willian, 20
4. Roberto Firmino, 19
5. Dusan Tadic, 18
6. David Silva, 14
7. Nathan Redmond, 14
8. Christian Eriksen, 13
9. Nathanial Clyne, 13
10. Erik Lamela, 13

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here