SHARE

NA MWANDISHI WETU

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/19 umemalizika jana, huku mabingwa watetezi, Simba, wakiendelea kutetea kiti chao walichokaa tangu msimu uliopita.


Tofauti na michuano kama hiyo iliyopita, msimu huu tumeshuhudia mabadiliko mengi katika soka la Tanzania, ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya mabao ya kufunga na vilevile ongezeko la timu kutoka 16 za awali na kuwa 20.


Pamoja na mengi ya kukumbukwa katika ligi hiyo, ni matukio mengi muhimu ya kisoka yaliyofanyika ndani ya Tanzania, ikiwamo michuano ya Afcon kwa vijana, pia timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kufuzu kucheza fainali za Afcon nchini Misri kuanzia Juni 21 – 19 Julai 2019.


Sisi Dimba tunapongeza juhudi kubwa za Serikali za kusimamia uendeshwaji wa michuano ya Afcon kwa vijana, pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi na wadau mbalimbali waliofanikisha jambo lolote lililosaidia kutufikisha hapa tulipo.


Aidha tunaipongeza Simba, hususan mwekezaji wake Mkuu, Mohamed Dewji kwa hatua mbili muhimu iliyofikia, kwanza kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia kufanikiwa kutetea ubingwa wake.


Kadhalika mahasimu wao, Yanga, ambao nao licha ya kukosa udhamini wa kutosha kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, lakini iliweza kupambana katika hali yoyote chini ya usimamizi wa kocha Mwinyi Zahera na kushika nafasi ya pili katika michuano ya Ligi.


Mara nyingi panapokuwa na mafanikio hapakosi changamoto, hivyo michuano hii nayo ilikuwa na dosari kadhaa, ikiwamo mabadiliko ya ratiba yaliyozikwaza timu, hasa za mikoani ambazo hazikuwa na udhamini na hivyo kuweza kucheza baadhi ya mechi katika wakati mgumu.


Ukiacha changamoto hiyo, ambayo sisi tunajua kwamba imezifanya baadhi ya timu kushindwa kushiriki vizuri, lakini pia hali ya kukosa udhamini katika michuano hiyo nalo liliongeza ugumu kwa timu shiriki kuweza kufanya vizuri.


Tunazipa pole timu zilizoaga mashindano hayo, hiyo haikuwa na jinsi, kwani utaratibu uko hivyo, jambo jema kwao ni kujipanga upya ili kuhakikisha zinarejea tena msimu wa mwingine kama utaratibu ulivyo.


Tunaamini kwamba, mengi makubwa tena yenye tija katika soka la Tanzania yaliyofanywa na TFF pamoja na tasisi nyingine yataangalia changamoto zilizojitokeza msimu huu na kuzifanyia kazi, ili zisiwepo tena msimu ujao.


Tunawatakia kila la heri wachezaji watakaobaki katika vikosi vyao, lakini hata wale watakaoacha waweze kupata timu nyingine na tuone tena wakipambana msimu ujao.


Dimba tunaamini ligi ijayo pia itakuwa na sura nyingi zaidi za vijana ambao ndio chimbuko la mafanikio ya soka letu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here