SHARE

LONDON, England

WAKATI Red Salzburg inaifuata Liverpool kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa Anfield, jina ambalo lilikuwa linaimbwa mno lilikuwa ni Erling Braut Haaland.

Tafsiri ya mtanange huo kwa kinda huyo ilikuwa ni nafasi yake ya kwanza kuuonyesha ulimwengu kwamba ana uwezo wa kuichachafya timu kubwa yoyote na hasa dhidi ya mabingwa watetezi wa Ulaya.

Haaland aliweza kufunga bao siku hiyo na baada ya mchezo huo kumalizika, habari zote zilimzungumzia yeye pamoja na mchezaji mwenzake wa Salzburg. Takumi Minamino. 

Dunia ilishuhudia namna kiungo mshambuliaji huyo raia wa Japan akiipa shida Liverpool kwa namna alivyokuwa akizunguka eneo kubwa la uwanja, akimaliza na asisti pamoja na bao moja. 

Achana na bao kali alilofunga mbele ya Virgil van Dijk na mlinda mlango wake, Alison Becker, kilichovutia wengi kutoka kwa Minamino ni kasi aliyonayo, umakini na jicho la kuiona nafasi ilipo na kuitumia ipasavyo. 

Minamino alikuwa ni mwiba. Alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafanya wachezaji wa Liverpool warudi nyuma na kila wakati alionekana kwenye ndani ya nafasi na alichachafya pande zote, kulia na kushoto.

Kila alipoupokea mpira alikuwa ni kama mnyama. Hakugeuka nyuma na hakulegeza kamba. Aliweza kukokota mpira kutoka eneo la timu yake, yadi 40 hadi langoni mwa timu pinzani. Njia pekee ya kumzuia ni kumuweka chini tu. 

Mechi ya pili tena dhidi ya Liverpool kule Austria, Minamino, 24, alifanya kweli. Alitumia vyema nafasi hiyo kujitangaza. Sawa na wenzake. 

Matokeo ya juhudi zao yameonekana. Wolverhampton imeripotiwa kumfukuzia mshambuliaji mwingine wa Salzburg, Hwang Hee-chan huku Man United na klabu nyingine za Serie A na Bundesliga nazo zikihusishwa na Minamino.

Hata hivyo, kwa mujibu wa gazeti la The Athletic, kuna uwezekano mkubwa wa Minamino kutua Liverpool mapema mwezi ujao na ikiwa taarifa hizo ni za kweli utakuwa ni uhamisho wa akili kubwa mno. 

Dau la pauni milioni 7.25 ndilo linalotosha kuvunja mkataba wake pale Salzburg. Kwa klabu za EPL hiyo ni fedha ndogo mno hasa Liverpool ambayo inawahitaji wachezaji wa kutosha wa aina ya Minamino.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ni muumini wa mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi kadhaa ndani ya uwanja. Minamino ni chaguo sahihi. 

Anacheza popote katika safu ya ushambuliaji. Namba 10 anacheza. Namba 8 anacheza. Aina yake ya uchezaji inarandana kwa kiasi kikubwa na ya Roberto Firmino. 

Majukumu wanayopewa na kuyatimiza katika nafasi tofauti ndio vitu vinavyowafananisha wawili hao na kubwa zaidi sio wachoyo wa pasi za upendo. Wachezaji wenye ubora wa aina hiyo wapo wachache mno duniani.

Bahati nzuri kwa Liverpool, wakifanikiwa kumnyakua rasmi Minamino watakuwa wamepata mrithi sahihi wa Firmino. Kingine kinachowaweka kwenye kundi moja ni ‘udhaifu’ wao katika suala la kufunga mabao ya kutosha.

Wakati Firmino akiachwa mbali na akina Mo Salah kwenye ishu hiyo ya kucheka na nyavu, Minamino naye hajaweza kuwa katika ramani sawa na Haaland ambaye ndiye injini kuu ya mabao pale Salzburg.

Ubora wa wawili hao hautegemei idadi ya mabao. Bali ni kitu gani wanachokifanya ndani ya mfumo wa timu na si kwamba hawafungi, wanafunga lakini katika uwiano unaoeleweka katika majukumu yao mengine.

Minamino ana mchango mkubwa katika upatikanaji wa mabao pale Salzburg. Takwimu zinaonyesha kuwa ana wastani wa kutoa pasi za mwisho 1.61 na asisti 0.32 kwa kila dakika 90.

Anapojaribu mashuti ni lazima asilimia 50 yalenge lango la mpinzani. Kumbuka pia yeye ni kiungo mshambuliaji hivyo anapokokota mpira hapaswi kuupoteza kizembe na Minamino kukokota mpira kwa mafanikio ya asilimia 50.

Anapopoteza mpira huwa si mchezaji mvivu kuutafuta. Ana takwimu ya kurudisha mpira katika himaya ya timu yake kwa asilimia 60 hasa katika eneo la mpinzani.

Liverpool watakuwa imetumia kiwango cha ziada cha akili yao kumchukua mtu huyu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here