SHARE

LONDON, England

KUELEKEA mtanange wa wapinzani wa jadi kutoka Jiji la Merseyside, klabu mbili za Liverpool na Everton, homa ya pambano lenyewe imeanza kupanda mara baada ya wachezaji wawili wa Everton kuumia kwenye mchezo uliozikutanisha timu zao za taifa za Ireland na Wales mwishoni mwa wiki hii.

Beki mahiri wa kulia, Seamus Coleman, alivunjwa mguu wake wa kushoto na beki wa Wales, Neil Taylor, huku kiungo James McCarthy, akishindwa kucheza kutokana na maumivu ya misuli ya paja.

Coleman anajulikana kwa uwezo wake mkubwa wa kushambulia na kukaba kwa wakati na hilo litakuwa pigo kubwa kwa kocha wa Everton, Ronald Koeman ambaye ataiongoza klabu yake hiyo hadi Anfield kuwavaa ndugu zao Liverpool.

Aidha, McCarthy ni mmoja wa viungo muhimu Everton ambapo katika eneo la kati yeye pamoja na Idrisa Gueye wameonesha ushirikiano mzuri na kuibeba timu sambamba na straika, Romelu Lukaku.

Maumivu ya msuli yanayomsumbua McCarthy yalitingisha uhusiano wa makocha wawili, Koeman na Martin O’Neill wa Ireland kwani Mdachi huyo aliwahi kumtaarifu O’Neill kuwa asimchezeshe kwenye mechi za kufuzu na jibu alilopewa Koeman ni kwamba hawezi kusikiliza ‘kelele za kijinga’.

Jumamosi ya Aprili 1 ndiyo siku ya mtanange wenyewe, Everton watahimili nguvu ya ndugu zao? Tusubiri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here