SHARE

NA HASSAN DAUDI

NI kweli Taifa Stars iliishia hatua ya makundi ya fainali za Mataifa Afrika mwaka huu (Afcon 2019) lakini hiyo haimaanishi kuwa kila kitu kiliishia pale. Bado kuna uhondo wa kutosha katika michuano hiyo inayoendelea kule Misri.

Ukiacha vigogo Cameroon, Morocco na wenyeji Misri kutoigusa robo fainali, maajabu mengine ni kikosi cha Madagascar. Ikiwa moja kati ya timu tatu ziliokwenda Misri kushiriki kwa mara ya kwanza fainali hizi, imetinga robo, ikiziacha Stars na Mauritania zikiishia makundi.

Juzi, wakiwa mbele ya mashabiki 20,000 wanaoujaza Uwanja wa Alexandria, Madagascar waliushangaza ulimwengu wa soka kwa kuwang’oa kwa penalti 4-2  moja ya timu zilizojaa nyota wanaocheza soka la kulipwa Ulaya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mchezo uliofikia hatua ya matuta baada ya sare ya mabao 2-2.

Kabla ya mtanange huo, Madagascar hawakuwa wakipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kwani katika mechi sita walizokuwa wamekutana na wapinzani wao walikuwa wametandikwa mara nne, wakishinda mbili tu.

Safari ya ajabu ya Madagascar

Kikosi cha Madagascar kilitarajiwa kuishia hatua ya makundi kwa kuwa hakikuwa na uzoefu lakini kilimaliza mechi zake za Kundi B kikiwa kileleni kwa pointi saba, mbele ya Nigeria (6), Guinea (4) na Burundi (0).

Kitendo cha Madagascar kuichapa Nigeria mabao 2-0 katika mchezo wa mwisho ndicho kilichowafanya wengi waanze kutowachukulia poa vijana hao wa kocha Nicolas Dupuis, mkufunzi raia wa Ufaransa.

Nigeria hawaamini unaambiwa

Kabla ya mchezo, hakuna ambaye angeweza kuiamini Madagascar mbele ya wa Nigeria. Si tu Nigeria hawakuwa wamepoteza mechi, pia hawakuwa wameruhusu nyavu zao kutikiswa tangu kuanza kwa michuano ya mwaka huu.

Pia, Nigeria walishinda mechi zote mbili walizowahi kuvaana na Madagascar, mitanange yote ikiwa ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afcon.

Lakini katika mchezo wa mwisho wa kundi lao, Madagascar walivunja uteja kwa kuichapa Nigeria mabao 2-0 na kuifanya dunia kushangaa na kuwaangalia kama timu ya kuogopwa licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye fainali hizo kubwa Afrika.

Stars haigusi kwa Madagascar

Labda mashabiki wa soka nchini wangependa Stars ipangwe na Madagascar kwenye kundi moja kule Afcon 2019. Kwamba, wangeiona kuwa ni timu nyepesi, sambamba na Benin, Mauritania na Kenya.

Lakini sasa, si tu kwa sababu ya kile wanachokifanya sasa nchini Misri, bali hata rekodi zinazonesha kuwa Madagascar ni mlima mrefu kwa Stars.

Katika mechi 10 kati ya pande mbili hizo, Stars wameshindi mara mbili pekee, wakipokea vichapo vitano na kuambulia sare tatu.

Kocha, nyota wa kulipwa

Mkuu wa benchi lao la ufundi ni Dupuis raia wa Ufaransa, ambaye kwa kuwa Madagascar hawana uwezo wa kumlipa kiasi cha fedha anachokitaka, pia ana kibarua huko nchini kwao, Ufaransa, akiwa ni sehemu ya benchi la ufundi la Fleury 91 inayoshiriki Ligi Draja la Nne.

Licha ya kwamba Ligi Kuu yao si yenye ushindani mkubwa, Dupuis anajivunia kikosi chake katika fainali za mwaka huu kwa kuwa kina wachezaji 11 wanaokipiga nchini Ufaransa.

Ukiacha kipa wao aliyekuwa langoni juzi dhidi ya DRC, Melvin Andrien, anayedakia FC Martigues ya Daraja la Pili huko Ufaransa, wana huduma ya nyota wa Lyon ya Ligue 1, Jeremy Michel Morel.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here