SHARE

LONDON, England

KWA mara ya kwanza kabisa kwenye historia ya Kombe la FA, hakutakuwa na mchezo wa marudiano kwenye hatua ya robo fainali, kama pambano likimalizika sare baada ya dakika 90.

Kanuni mpya za mashindano zinaelekeza kuwa, sasa ni lazima mshindi apatikane. Ngoma ikienda sare kwa dakika 90, zitaongezwa dakika 30 na kama bado hakuna mshindi, changamoto ya mikwaju ya penalti ndiyo itakayomaliza mzizi wa fitna.

Na sasa makocha wataruhusiwa kufanya ‘sub’ ya mchezaji wa nne pindi mchezo unapoingia kwenye dakika 30 za nyongeza, kanuni hii itatumika kwenye michezo ya robo, nusu na fainali.

Mfumo kama huu ulitumika msimu uliopita kwenye michuano ya Copa America, baada ya kubuniwa na bodi ya kimataifa ya soka, Amerika Kusini (IFAB).

Hivyo Chama cha Soka England (FA) kimetambulisha kanuni hii mpya ikiwa ni sehemu ya kuiongezea msisimko michuano hii ya FA.

Kanuni hizi zitatumika kwenye pambano la kesho baina ya vinara wa Ligi, Chelsea watakuwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Stamford Bridge kuikaribisha Manchester United, kwenye pambano lililojaa visasi na hamasa ya aina yake.

Hii ni mara ya pili msimu huu kwa wawili hawa kukutana, baada ya awali Chelsea walipoichapa United bao 4-0, kwenye mchezo wa Premier League.

United wataingia kwenye pambano hili wakimkosa straika wao, Zlatan Ibrahimovic, aliyefungiwa mechi tatu na FA kwa kosa la kumpiga kiwiko beki wa AFC Bournemouth.

Chelsea kwa upande wao wana ndoto za kubeba mataji mawili msimu huu, hivyo hawatakuwa na huruma mbele ya United kwa kupanga full mziki wao unaotisha nchini England msimu huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here