SHARE

NA SAADA SALIM

UKITAKA kukosana na mashabiki wa Yanga, mseme vibaya kiungo wao, Mkongomani Papy Kabamba Tshishimbi, miongoni mwa wachezaji vipenzi kutoka kwa mashabiki kutokana na uwezo wake anaouonyesha akiwa uwanjani.

Tshishimbi alisajiliwa na Yanga akitokea Mbabane Swallows ya Swaziland katika msimu wa usajili wa dirisha kubwa, ambao unatajwa kuwa umekuwa na faida.

Sasa si utulivu na usafi wa uwanjani pekee, bali mchezaji huyo amekuwa wa kipekee zaidi hata katika maisha yake nje ya uwanja, kwani hata chakula chake huwa kinakuwa cha kipekee.

Katika mazungumzo yake na BREAKING NEWS, kiungo huyo amethibitisha kwamba, katika kitu ambacho amekishindwa ni kula chakula cha mapishi ya Kitanzania.

Anasema mara nyingi amekuwa akijitahidi kujaribu kula chakula kinachoopikwa na Watanzania, lakini ameshindwa, hali hiyo imepelekea kujinunulia chakula na kupika mwenyewe.

“Siwezi kula mapishi ya Kitanzania, yamenishinda, hivyo nalazimika kupika chakula mwenyewe kwa kuzingatia mapishi ya Kikongoman, hali hiyo nafanya hata nikiwa kambini,” anasema Tshishimbi.

Tshishimbi anasema kulingana na kutofurahia chakula cha Tanzania, inamlazimu kujipikia chakula kila anapokwenda, hasa akiwa kambini na timu yake hiyo.

MAZINGIRA YA TANZANIA:

Kiungo huyo anasema katika suala la mazingira na maisha mengine hayana tofauti, kwani ameweza kuyazoea mapema kutokana na wenyeji wake kuishi naye vizuri na kumpa ushirikiano wa hali ya juu.

“Haina shida, kama ilivyo kwa chakula, kwani ukiangalia suala la chakula imekuwa shida, lakini si katika mazingira ya kuishi,” anasema Tshishimbi.

MCHEZAJI WA MECHI KUBWA:
Anasema kulingana na mechi alizocheza, anatamani apangwe katika mechi kubwa, ikiwamo mechi na Simba na zile za kimataifa, kutokana na aina ya uchezaji wa wachezaji wa timu hizo.

“Hizi timu nyingine ni tatizo kutokana na jinsi wachezaji wanavyokamia na kucheza rafu, hali ambayo nahofia kuumizwa na kupata majeraha,” anasema.

Tshishimbi anasema suala la kucheza kwa rafu kwa wachezaji wa timu ndogo linamfanya kutamani kucheza na Simba au timu kubwa kutokana na utulivu wa wachezaji wa timu hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here