SHARE

NA SAADA SALIM           |          


KIKOSI cha Simba jana kilifunga rasmi kambi yake ya mazoezi nchini Uturuki, tayari kurejea nchini kesho kwa ajili ya maandalizi ya mechi yake dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana.

Timu hizo zitaumana Jumatano ya Agosti 8, mwaka huu, katika mchezo wa kirafiki kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya Simba Day, inayoadhimishwa kila mwaka na klabu hiyo.

Kule Uturuki, Simba itakuwa na kumbukumbu nzuri katika kambi yao waliyoiweka kwa takriban wiki mbili na kucheze mechi mbili za kirafiki dhidi ya Waarabu kutoka Morocco.

Walianza kucheza dhidi ya MC Oujder, inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na jana walicheza dhidi ya Ittihad Riadi de Tanger, ambao ndio mabingwa wa Ligi ya nchi hiyo.

Moja ya mafanikio ya ziara hiyo, kwanza ni kupata kambi yenye utulivu ambayo kocha wake msaidizi, Masoud Djuma aliisifu kuwa imewawezesha kuinoa timu vizuri tayari kwa pambano lolote litakalokuja mbele yao, iwe la ndani au la kimataifa.

Lakini kama haitoshi, timu hiyo imeweka historia kwa wenyeji, ambapo mara kadhaa walishuhudia sura za mawakala wa soka kutoka pande mbalimbali za nchi hiyo wakifuatilia mazoezi ya timu hiyo.

Miongoni mwa wachezaji wa kikosi hicho ni Shiza Kichuya na Salamba, ambao mara nyingi walikuwa kivutio mazoezini, lakini pia kuwavutia mawakala.

Haikuwa rahisi kujua endapo kuna mipango yoyote iliyofanywa na klabu hiyo kwa ajili ya kuwaunganisha wachezaji wake na mawakala kutokana na udhibiti mkubwa uliokuwa katika kambi ya timu hiyo.

Msimu huu klabu hiyo chini ya ufadhili wa mfanyabiashara Mohamed Dewji, imeweka wazi kwamba inataka kufanya mapinduzi kwa kuiondoa klabu hiyo katika mtazamo wa kitaifa na kuifanya ya kimataifa.

Kwa kuanza kutekeleza majukumu hayo, Kaimu Rais wake, Salim Abdala ‘Try Again’, alisema wataanza kutunisha mfuko kwa kufanya mauzo makubwa ya jezi katika tamasha la Simba Day, lakini pia watalipa umuhimu wa kipekee suala la ujenzi wa uwanja utakaotumiwa na timu hiyo kwa ajili ya mazoezi pamoja na mechi za ndani na za kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here