SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

WAKATI baadhi ya ligi kubwa barani Ulaya zikitarajia kwenda mapumziko ya siku kadhaa kwa ajili ya kusherekea sikukuu za Krismasi na kuukabisha mwaka mpya wa 2017, huku wachezaji pamoja na makocha wakijumuika na familia zao, Ligi Kuu ya England itakuwa ikiendelea kuwasha moto kama ilivyo kawaida ya misimu yote.

Hata hivyo katika ligi hiyo inayofuatiliwa kwa karibu na mamilioni ya mashabiki ulimwenguni kote kutokana na soka lake kuwa la kibiashara, makala hii inakuletea mitanange mikali ya muda wote iliyosisimua ikiwa kama fainali.

 

Chelsea 2-2 Tottenham, 02/05/2016

Tottenham ikiwa kwenye mbio za ubingwa ikifukuzana kwa karibu sana na Leicester City, ilijikuta ndoto zao zikizimwa katika hatua za mwisho mwisho na ‘The Blues’ baada ya kukubali  sare ya mabao 2-2.

Mchezo huo ulikuwa ni kama vile fainali, kutokana na kasi na ubunifu wa hali ya juu wa aina yake. Eden Hazard ndiye aliyefanikiwa kuibuka shujaa wa mchezo baada ya kusawazisha bao la pili dakika za lala salama lililoibua shangwe kubwa jukwaani na kuwafanya Leicester kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu England msimu huo kwani tayari Spurs wasingeweza kuwafikia kwa pointi.

 

Newcastle 5-0 Man United, 20/10/1996

Kilikuwa kiama cha mabao kwa Manchester United kukutana nacho kutoka kwa Newcastle United, ambapo mlinda mlango mahiri wa Mashetani hao Wekundu Peter Schmeichel, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuokoteshwa mpira nyavuni mara nyingi msimu huo, ingawa awali huko nyuma alikuwa na  rekodi nzuri ya kucheza michezo mitano bila kuruhusu nyavu zao kuguswa.

Mshambulijia matata wa Newcastle Alan Shearer aliitikisa wavu mara mbili, kama ilivyokuwa kwa nyota mwenzake Les Ferdinand, lingine moja likifungwa kwa umbali wa mita 25 kutoka mguuni mwa Philippe Albert.

Bosi wa kipindi hicho wa klabu hiyo kutoka viunga vya St James Park, Kevin Keegan alikuliwa akisema; “Hii ni historia itakayodumu miaka nenda rudi. Kuifunga timu kubwa na ngumu kama Manchester United, nawapongeza vijana wangu.”

 

Leicester 3-3 Arsenal, 27/08/1997

Washika Mitutu wa jiji la London, Arsenal wakiwa ugenini dhidi ya Leicester City, huku pia wakiwa kwenye kiwango chao cha hali ya juu, walikuwa wa kwanza kuingia kimiani mara mbili, mabao yote yakifungwa na Dennis Bergkamp, kabla ya Emile Heskey na Matt Elliot kusawazisha.

Licha ya Bergkamp kuifungia timu yake bao la tatu kwa kumpiga chenga maridadi beki wa Leicester, lakini dakika za nyongeza (93) vijana wa kocha Arsene Wenger walijikuta wavu wao unatikiswa kwa mara nyingine ukiwa ni mpira wa kichwa wa Steve Walsh.

 

Newcastle 4-4 Arsenal, 05/02/2011

Straika wa Newcastle Andy Caroll anatajwa kuwa ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo huu, ambapo hata baada kumalizika mchezo alimwagiwa sifa za kutosha na kocha wake Alan Pardew.

Hiyo ilitokana na kuivuruga vilivyo beki ya Arsenal, ikichagizwa na pengo la kiungo wao Abou Diaby aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwa kitendo cha utovu wa nidhamu, akimchezea rafu mbaya Joel Barton na kumsukuma Kevin Nolan.

Awali kipindi cha kwanza cha mchezo huo, Arsenal walionekana kuwa bora na kufanikiwa kuwachakaza wapinzani wao hao vilivyo na kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza kwa mabao 4-0, lakini kipindi cha pili Newcastle walitakata vilivyo ikichagizwa na ubora wa Cheik Tiote kwenye safu ya kiungo na kufanikiwa kusawazisha mabao yote, na mchezo kumalizika kwa sare ya 4-4, mawili yakiwa ya penalti baada ya Barton na Leon Best kuangushwa ndani ya boksi.

 

Aston Villa 1-2 Man United, 23/08/1993

Vijana wa Sir Alex Ferguson wakiwa kwenye mbio za ubingwa mzunguko wa kwanza hawakuwa na masihara katika kuhakikisha wanapata matokeo chanya.

Wakiwa wageni wa Aston Villa, waliacha vilio kwa mashabiki mahali hapo, katika kipindi hicho ambapo Villa ilikuwa ikionekana kuwa miongoni mwa timu ngumu inapokutana na vigogo wa ligi hiyo, lakini wakajikuta wakiambulia vumbi mbele ya United waliofanikiwa kukusanya pointi tatu katika viunga vya Villa Park.

Hatari zaidi ilikuwa kwenye eneo la kiungo, lililotawaliwa kwa kiasi kikubwa na fundi Lee Sharpe,  aliyefunga bao murua, akitumia vema pasi ya Ryan Gigs. Bao jingine la Mashetani Wekundu katika mtanange huo lilifungwa na Paul Ince.

 

Tottenham 3-5 Man United, 01/10/2001

Tottenham wakiwa katika dimba lao la nyumbani White Hart Lane, walionyesha ubora wa hali ya juu, ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, walifanikiwa kuinyoosha Manchester United na kwenda katika vyumba vya kubadilishia nguo wakiongoza kwa bao 3-0, maabao yakifungwa na Dean Richards, Les Fernand na Christian Ziege.

Lakini kipindi cha pili kocha wa Mashetani Wekundu enzi hizo, Sir Alex Ferguson, alionyesha maajabu yake kwa kuwapa maelekezo maalumu wachezaji wake kwa kuwaambia walichopaswa kukifanya muda huo ili kupindua matokeo, ambapo ilikuwa ni dakika za awali tu za kipindi hicho Andy Cole alitikisa vyavu  na kufungulia mvua hiyo ya mabao kupitia kwa Laurent Blanc, Ruud van Nistelrooy, Juan Sebastien Veron na David Beckham.

 

Manchester City 3-2 QPR, 13/05/2012

Wakati ikiwa ni mechi ya mwisho kabisa za msimu wa Ligi Kuu England, huku timu mbili mahasimu Manchester United na Manchester City zikiwania ubingwa hatua hizo za lala salama, ilikuwa ni City  ya kocha Roberto Manchin aliyenyakuwa mwali huyo kwa kumbamiza QPR mabao 3-2, mchezo ambao ulikuwa kama fainali, ushindi ukipatikana dakika  mwisho za jioni kabisa jua kuzama likiwamo bao la funga kazi la Kun Aguero.

Katika upande wa pili mahasimu wao Manchester United ambao muda huohuo walikuwa wakikipiga dhidi ya Sunderland, licha ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililotiwa kimiani na straika wao Wayne Rooney, halikuwasaidia kutokana na kuachwa pointi mbili nyuma na City aliyotwaa kombe hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here