SHARE

JESSCA NANGAWE

ENDAPO Simba wanataka kuimarisha kikosi chao kuelekea katika ndoto ya kucheza michuano ya kimataifa hapo mwakani, basi wawe makini sana katika suala zima la usajili.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba kikosi hicho kina wachezaji wengi wakongwe waliocheza kwa kipindi kirefu na hivi sasa wakielekea kuchoka.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha, muda mfupi kabla ya kukabidhiwa jukumu la kuisuka upya klabu hiyo aliwahi kuzungumzia hilo akisisitiza miungoni mwa jukumu zito atakalolifanya ni kuhakikisha wachezaji chipukizi wanapata nafasi kikosini.

Hata hivyo zoezi hilo hakuweza kulikamilisha kwa asilimia kubwa kutokana na kutohusika moja kwa moja katika usajili uliopita.

Sasa mchongo wa usajili katika klabu hiyo umeanza mdogomdogo huku mawakala wakiifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa katika kipindi hiki ambacho michuano ya ligi imesimamishwa kutokana na kuzuka kwa janga la virusi vya corona.

Habari kuhusu mchakato wa usajili kuanza kimyakimya umeanza kuwafikia wachezaji mbalimbali hususan wale wenye marafiki zao wanaocheza katika timu za hapa nchini Tanzania.

Miungoni mwa wachezaji waliofikiwa na habari njema kutoka klabu ya Simba ni raia wa Nigeria, Victorien Adebayor, ambaye kwasasa anakipiga nchini Ghana katika klabu ya International Allies Football Club.

Mido huyo ambaye inasemekana anafahamiana vizuri na aliyekuwa kiungo wa Simba, James Kotei, anaitaka Simba baada ya kupata mchongo kutoka kwa ofisa mmoja wa klabu ya Madema ambaye amekuwa na uhusiano mzuri na klabu ya Simba.

Akizungumza na DIMBA Jumatano kwa njia ya mtandao, Adebayor alikiri kuifahamu Simba kupitia rafiki yake wa karibu, Kotei, na akasisitiza endapo klabu hiyo itamuhitaji hatosita kujiunga nayo kwa kuwa anatamani sana kucheza Tanzania.

Endapo Simba itanasa saini ya nyota huyo, itakuwa imeongeza wapachika mabao wazuri na vijana kwani mchezaji huyo amefikisha umri wa miaka 23 na ana kiwango kizuri cha ufungaji.

Katika msimamo wa ligi yao, timu yake ipo nafasi ya 10 kati ya timu 18 lakini yeye akifanikiwa kuwa mchezaji bora wa mwezi uliopita akiwa amefunga mabao saba na jumla anayo mabao 11 katika orodha ya wafungaji bora huku akitoa pasi tano za mabao. Adebayor pia amecheza kwa mafanikio makubwa katika klabu ya AS Douanes kuanzia mwaka 2014 hadi 2017 ikiwa inashiriki Ligi Kuu ya Nigeria na baadaye akajiunga na US Raon ya Ufaransa kisha AS Gnn kabla ya kutua Inter Allies anayocheza kwa sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here