SHARE

JESSCA NANGAWE

UNAAMBIWA mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, kinda wa Simba, Miraji Athuman, alikua mchezaji aliyesubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka Mkoani humo huku wengi wakitaka kupiga naye picha.

Simba ambao ni vinara wa ligi hiyo, leo itakua ugenini kwenye Uwanja wa Shekh Amri Abeid ikivaana na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nyota huyo wa Simba ambaye kwa sasa ni kipenzi cha mashabiki wengi ameendelea kupata jina kutokana na kiwango chake kuendelea kukua siku hadi siku.

Miraji ambaye ni kipenzi cha kocha wake, Patrick Aussems, alianza kung’ara katika mechi za awali za ligi akitokea benchi na kuwapa shangwe mashabiki wa timu hiyo.

Mpaka sasa nyota huyo amefunga mabao matatu tangu kuanza kwa ligi hiyo huku akifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora mwa mwezi Septemba sambamba na kocha wake Aussems.

Kwa mwezi huo wa Septemba, Simba ilicheza michezo mitatu na kushinda yote ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Kagera Sugar mabao 3-0 na Biashara United mabao 2-0.

Kinda huyo ambaye alitua Simba akitokea Lipuli FC, alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio hayo ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mabao mawili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here