SHARE

MADRID, Hispania

SOKO la usajili miaka ya karibuni limekuwa la gharama kubwa sana, wachezaji wamekuwa wakipatakana kwa bei za juu kama ilivyoonekana kwa Neymar wakati anatoka Barcelona kwenda PSG, mwaka 2017.

PSG walilipa kitita cha pauni milioni 198, kwa kifupi walivunja kipengele cha malipo ya Neymar kilichowekwa na wababe hao wa Ligi Kuu Hispania, La Liga.

Hata hivyo, hivi sasa inaonekana kuwa jambo tofauti kwani timu zimekuwa zikiweka vipengele vikubwa vya ada ya uhamisho kwa wachezaji wao ili wapinzani washindwe kunasa saini zao.

Makala haya yanakuletea wachezaji watano ambao wana vipengele ghali zaidi katika mikataba yao duniani.

LIONEL MESSI

Wala haishangazi kumuona staa wa Barcelona, Lionel Messi katika kundi hili. Mchezaji huyo anayetumia mguu wa kushoto ni mmoja wa wachezaji bora duniani, ndio maana timu hiyo yenye maskani yake Uwanja wa Camp Nou wameweka kiasi cha pauni milioni 592.5 kwenye mkataba wake.

Wachezaji wengine wanaofanana thamani hiyo na nyota huyo wa Barcelona ni Isco, Marco Asensio na Vinicius Junior wote wa Real Madrid.

Inaweza isiwe rahisi kwa timu kuvunja kipengele hicho kilichopo katika mkataba wa Messi lakini staa huyo ameonesha nia ya kutaka kuondoka Barcelona.

BRAHIM DIAZ

Diaz ni mmoja wa vijana wenye vipaji vikubwa, ndio maana Real Madrid hawakusita kutoa kiasi cha pauni milioni 15.5 kuinasa saini yake kutoka Manchester City, kwa ajili ya kijana huyo wa miaka 20.

Licha ya kumpata kijana huyo mdogo, mabingwa hao wa Ulaya mara nyingi zaidi wameweka kipengele kizito zaidi katika mkataba wake, hiyo inaonesha ni jinsi gani wanataka kumwona Santiago Bernabeu kwa muda mrefu zaidi.

Timu yoyote itakayohitaji huduma ya Diaz italazimika kutoa kiasi cha pauni milioni 634.9 ili kuvunja mkataba uliopo Santiago Bernabeu.

Hata hivyo, Diaz bado hajafanikiwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid, itakuwa ngumu kwa timu kuhitaji huduma yake sababu bado hajathibitisha uwezo wake.

LUKA MODRIC

Mshindi wa tuzo ya Ballon díOr mwaka 2018, amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika klabu na nchi yake kwa ujumla miaka ya karibuni.

Itakumbukwa wakati Real Madrid wanashinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya alikuwa mchezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Zinedine Zidane, ndio maana waliweka kipengele cha pauni milioni 634.9 kwa staa huyo wa Croatia mwenye umri wa miaka 34.

Tangu ajiunge na kikosi hicho, Modric aliisaidia timu hiyo kupata mafanikio kwa kushinda mataji ya La Liga, Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo waliweka rekodi kwa kutwaa mara tatu mfululizo.

ANTOINE GRIEZMANN

Barcelona walimsajili Griezmann kutoka Atletico Madrid dirisha kubwa lililopita kwa kuvunja mkataba wake uliokuwa na kipengele cha pauni milioni 105. Lakini vinara hao wa Ligi Kuu Hispania, La Liga, wameweka kiasi cha pauni milioni 677.2 kwa nyota huyo mshindi wa Kombe la Dunia.

Wababe hao wa Catalunya wanaamini Griezmann atakuwa msaada mkubwa katika kikosi hicho hata kama Messi ataamua kuondoka ndani ya timu hiyo ndio maana wamempa mkataba wa miaka mitano wa kuwepo Camp Nou.

KARIM BENZEMA

Inashangaza kidogo, mchezaji mwenye kipengele kikubwa zaidi dunia cha uhamisho ni straika wa Real Madrid, Karim Benzema ambaye kiasi chake ni pauni milioni 846.7.

Staa huyo raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 32 yupo Santiago Bernabeu kwa zaidi ya miaka 10 sasa na amedhihirisha kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa timu hiyo tangu alipoondoka mfungaji wa mua wote wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here