SHARE

NA MWANDISHI WETU


KAIMU kocha mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwassa, amesema laiti muda ungeongezwa kwenye pambano lao la watani wa jadi, basi wangeshinda.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Januari 4, 2020 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Saalam, Yanga ilitoka nyuma na kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba.
Akizungumza mara baada ya kumalizika mchezo huo uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki, Mkwassa aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kuondoka na pointi moja.
Alisema baada ya kwenda mapumziko kipindi cha kwanza huku Simba wakiwa wanaongoza, aliwataka wachezaji wake wasivunjike moyo.
“Wao (Simba) wamekuwa pamoja kwa muda mrefu ila nawapongeza wachezaji wangu kwa kurudi mchezoni licha ya kuwa nyuma kwa mabao mawili na baada ya kusawazisha mabao yote tulianza kuutawala mchezo hivyo zingeongezwa muda tungefunga la tatu,” alisema Mkwassa.
Naye kocha wa Simba, Sven Vandenbrook, alisema mabao ya Yanga yalifungwa wao wakiwa pungufu uwanjani.
“Mchezaji wetu alipata jeraha na alikuwa nje akitibiwa na hiyo ikawapa mwanya kufunga mabao hao, naamini hilo lisingewezekana kama tungekuwa 11 uwanjani,” alisema Mbelgiji huo.
Mabao ya Simba yalifungwa na Meddie Kagere na Deo Kanda huku yale ya Yanga yakiwekwa kimiani na Mapinduzi Balama na Mohammed ‘MO’ Banka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here