SHARE

NA WINFRIDA MTOI

MWEKEZAJI na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameitisha faili la usajili mpya wa timu hiyo aanze kulifanyia kazi fasta.

Taarifa za kutaka kurejea kwa baadhi ya ligi duniani zikiwemo za barani Afrika zimemshtua Mo na kupanga kutumia kipindi hiki kukamilisha dili zote za usajili uliopendekezwa katika ripoti ya kocha mkuu wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck.

Awali tajiri huyo alikuwa kama amepotezea mipango hiyo kutokana na janga la virusi vya corona akiamini huenda michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika isifanyike. Lakini kurejea kwa Ligi mbalimbali kumeleta matumaini kuwa michuano ya CAF itafanyika huku Simba wakitarajia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.

Simba imepanga kufanya usajili ikilenga zaidi nyota wanaoweza kuwapa mafanikio katika michuano ya kimataifa kwa sababu kikosi chao tayari kimeonesha ubora kwa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo DIMBA imezipata kutoka ndani ya Simba, Mo amemtaka Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mbatha, kuhakikisha anamkabidhi mafaili ya wachezaji wote wanaotakiwa.

Mtoa taarifa huyo alisema Senzo ameshakaa mara kadhaa na kocha mkuu wa Simba, Sven kujadiliana wachezaji wanaofaa kutua kikosini hapo.

Inadaiwa kuwa tayari, Sven ameshakabidhi kila kitu ikiwamo ripoti na kilichobaki ni utekelezaji wa kuletewa wachezaji anaowataka kulingana na nafasi alizopendekeza.

“Haya mambo ya kusikia ligi inafutwa, mara mashindano ya CAF, yalitukatisha tamaa katika suala la usajili, hata bosi wetu, Mo, alikuwa hana mzuka, lakini juzi ameomba kupelekewa majina.

“Ametaka faili la majina ya wachezaji wote wanaotakiwa kuwepo katika kikosi cha Simba msimu ujao, wapya na wale waliopo ambao mikataba yao inamalizika,” kilisema chanzo hicho.

Kati ya wachezaji wanaotajwa katika usajili wa Simba ni wazawa Bakari Mwamnyeto na kiungo wa Namungo FC, Lucas Kikoti, huku moja wa wageni akiwa ni straika Sogne Yacouba wa Asante Kotoko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here