SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

UKISIKIA mkwara mzito ndio huu. Bilionea wa Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji, amefunguka kuhusu mkakati wake wa kuifanya timu hiyo iwe tishio zaidi barani Afrika kwa kuahidi kutoa mkwanja mrefu ya kusajili mchezaji yoyote atakayependekezwa na benchi la ufundi bila kujali gharama.

Mo Dewji ni kama anajibu mapigo kwa mahasimu wao wa jadi kisoka, Yanga, kupitia kwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Mhandisi Hersi Said, ambaye alijinadi kuwa wamejipanga kufanya usajili wa nguvu utakaotikisa barani Afrika ili kutimiza ndoto za kuiona timu hiyo ikifanya makubwa kimataifa.

Kauli za Mo Dewiji na Hersi ni kama zimekoleza mbio za usajili kwa vigogo hao wa soka nchini kuonyeshana jeuri ya fedha kwa kila mmoja kujipanga kuboresha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

Akitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mo Dewji jana aliandika kwamba watasajili mchezaji yeyote kutoka sehemu yoyote kutokana na mahitaji ya kocha wao na watashuka kwa kishindo kwani wao hawana maneno mengi.

Mbali na hayo, Mo Dewji alikwenda mbali zaidi na kuwahakikishia mashabiki wa Simba kwamba hakuna mchezaji yeyote atakayeondoka Simba ikiwa ni kumaanisha wachezaji waliopo hawatakiwi kuwa na wasiwasi wowote.

“Wanasimba wenzangu, nataka niwahakikishie hakuna mchezaji wetu yoyote atakayeondoka Simba, lakini pia tutasajili mchezaji yoyote, kutoka popote kama mwalimu wetu atamuhitaji kwenye kikosi chake. Tutashuka kwa kishindo, hatuna maneno mengi lakini tupo,” alisema.

Baada ya kutupia maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook, mashabiki wengi wa Simba walionekana kujawa na furaha huku wengine wakienda mbali zaidi na kudai kwamba hakuna timu itakayosogeza mguu mbele yao.

Mmoja wa mashabiki wa Simba, Zuberi Makale, alisema: “Naamini wewe ndio mwenye uwezo wa kufanya hivyo kwa sababu mpira unaujua sio wengine wanalazimisha.”

Baadhi ya mashabiki hao wameonekana wazi wakimtaka bosi wao huyo kuwarejesha kundini mastaa wao wawili, Emmanuel Okwi pamoja na James Kotei ambao waliichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa.

Simba kupitia kwa Mkuu wao wa Habari na Mawasiliano, Haji Manara, alisema mpango walionao ni kuhakikisha wanachukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 10 mfululizo na kauli hiyo ya Mo Dewji inaashiria kile kilichosemwa na msemaji wao huyo.

Mpaka sasa, Simba imeshatwaa ubingwa mara mbili mfululizo na msimu huu wanayo nafasi kubwa ya kuutwaa kwa mara ya tatu kwani wakishinda michezo mitano kati ya 10 waliyobakisha, watafikisha jumla ya pointi 86 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Kikosi hicho Jumapili inayokuja kitakabiliana na Ruvu Shooting katika mwendelezo wa ligi hiyo ambayo ilisimama kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na janga la corona.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here