SHARE

NA HENRY PAUL

JINA la golikipa mahiri, Morris Nyuchi, si geni kwa wapenzi wa soka nchini, hususan wa klabu ya Nyota Nyekundu ya Dar es Salaam, kwani wamemwona mkongwe huyo akichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa katika miaka ya 1980.

Umahiri wa mlinda mlango huyo ulitokana na aina ya udakaji wake, kwani alikuwa anadaka michomo mikali kwa staili ya mbwembwe na kuwafanya washambuliaji kukata tamaa.

Mkongwe huyo ambaye hivi sasa amejikita katika kazi ya ukocha, pamoja na kuichezea Nyota Nyekundu kwa mafanikio, pia katika vipindi tofauti amezichezea timu kadhaa ikiwemo Yanga, JKT Makao makuu na Urafiki ya Dar es Salaam.

Hivi karibuni DIMBA Jumatano, lilikutana na nyota huyo wa zamani, ambaye hivi sasa ni Mkufunzi wa Michezo wa Shule ya Sekondari Chamazi Islamic na kufanya naye mahojiano kuhusiana na nini kifanyike ili kuinua kiwango chetu cha soka ambacho hivi sasa kinaonekana kusuasua.

Katika mahojiano hayo, Nyuchi anatoa maoni yake akisema:

“Pamoja na kwamba kuna sababu nyingi zinazosababisha kiwango chetu cha soka kuzidi kudidimia siku hadi siku, lakini moja ya sababu kubwa ni kwamba klabu zetu kuendelea kuweka mkazo katika kuwategemea wachezaji wenye umri mkubwa badala ya kuweka mkazo katika kuwekeza soka kwa vijana.

“Kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo ndio njia pekee na sahihi ambayo kwa kiasi kikubwa inawezesha kuinua kiwango cha soka kwa klabu na nchi husika kwa ujumla.

“Mfano mzuri wa kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo, tumehushuhudia katika nchi nyingi zilizoendelea kisoka, kwani nchi hizo ziligundua mapema na kuanza kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo na kuachana kabisa na wachezaji wenye umri mkubwa.

“Hata nchi za Afrika Magharibi kama Ghana, Nigeria, Cameroon, Ivory Coast na hata Senegal, zimekuwa na kiwango kizuri cha soka baada ya kuanza kuwekeza soka kwa vijana na kuanzisha shule za kufundishia mchezo huu ‘academies’.

“Mbali na nchi hizo za Afrika Magharibi kupiga hatua kisoka, pia hata nchi za Ulaya kama vile Hispania, Uholanzi, Brazil, Ujerumani, Croatia na England nazo zimesonga mbele kisoka baada ya kuona umuhimu wa kuwekeza soka kwa vijana.,

“Hivyo na sisi kama tunataka kutoka hapa tulipo na kusonga mbele kisoka hatuna budi kuanza kuwekeza kikamilifu soka kwa vijana na kuachana kabisa kukumbatia wachezaji wenye umri mkubwa.

“Kwa upande mwingine kama Tanzania tunataka kuinua kiwango chetu cha soka ni vyema Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuangalia uwezekana wa kurudisha michezo kazini.

“Nakumbuka kipindi cha nyuma sehemu za kazi kulikuwa na timu zenye viwango bora ambazo kwa kiasi fulani maendeleo ya soka nchini kama Pamba ya Mwanza, Ushirika ya Moshi, Sigara na Pilsner za Dar es Salaam, Tumbaku ya Morogoro, Ndovu ya Arusha, CDA na Waziri Mkuu za Dodoma na Pamba ya Kigoma. “Timu hizo ambazo karibu zote zilikuwa Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), kutokana na kuwa na wachezaji mahiri, kiwango cha soka nchini kwa kiasi fulani kilikuwa juu, hivyo ni vyema kurudisha tena sera hiyo ya michezo kazini kama ilivyokuwa zamani

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here