SHARE

NA AYOUB HINJO

ALIPIGA hatua zake taratibu na kuelekea kule ambako kulikuwa na miguu ya meza iliyosimamishwa juu ya meza nyingine. Kwa mbali, hofu ilitanda katika akili yake, mapigo ya moyo yaliongezeka kasi kila aliposogea mbele kufuata kivuli kile.

Alianza kwa kuona viatu vyeusi na suruali nzuri iliyooonekana kushonwa kwa utulivu na fundi, kisha aaliona koti jeusi likiwa limefika usawa wa magoti ya suruali hiyo iliyonyoosheka kweli.

Aliona mtu akiwa amesimama huku uso wake ukipambwa na tabasamu, mtu aliyeonekana kufurahi huku macho yake yakionesha mshangao kwa yule aliyekutana naye wakati ule.

Kwa mara ya nyingine tena, aliweza kukanyaga ardhi ya Malkia Elizabeth baada ya kipindi kifupi kupita alionekana akitoa dozi katika Jiji la Manchester.

Ilikuwa furaha kwake na Roman Abramovich ambaye alidhani amevamiwa na jamabazi, inaaminika Jose Mourinho alikuwa wa kwanza kufika katika boti ya kifahari ya tajiri huyo.

Alitulia, kwa shahuku kubwa mara zote alionekana akiiangalia saa yake, muda ulikuwa hauendi, kama mishale ya sekunde ilikuwa imebebwa na kobe. Haikuonekana kusogea kabisa.

Yote hayo yalitokea baada ya Mourinho kutimiza ndoto yake ya kufundisha soka nchini England. Mwisho wa siku, ilikuwa sehemu pekee aliyoweka heshima kwa kusimama katikati ya Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger kimafanikio.

Ni nani asiyemfahamu Mourinho? Nadhani hakuna, kuanzia watoto wadogo, akina mama na hata wazee ambao si wafuasi wa mpira wanamfahamu kocha huyo mwenye maneno mengi na mafanikio katika timu alizopita.

Mbinu ni kitu pekee ambacho Mourinho amekuwa nacho kwa muda mwingi na kitu kikubwa kwake amezoeleka katika falsafa za uzuiaji “parking bus” na kushambulia kwa kushtukiza.

Mbinu hizo zimempa umaarufu zaidi na mara nyingi alifanikiwa kupata alichohitaji kutokana na kundi la wachezaji aliokuwa nao kutii kila alichokihitaji ndani ya uwanja.

Lakini katika timu zote ambazo amepita, Mourinho alifanikiwa kuwa na mchezaji ambaye alimfanya kuwa karibu yake, alikuwa muhimu kwake na kila kitu chache ndani ya uwanja.

Alipotangazwa kuwa kocha wa Tottenham, wapo waliotabiri kuwa kuna wachezaji ambao hawataweza kupata nafasi kwa Mreno huyo, labda kutokana na aina ya soka ambalo amekuwa akifundisha.

Mara zote, Mourinho hutumia wachezaji waliotayari kujitolea kwa ajili yake na timu, ambao hawatajali maslahi binafsi kwanza.

Spurs ambayo imezungukwa na wachezaji wenye uwezo na ubora mkubwa, pengine kuliko timu zingine za England au Ulaya, Mourinho ameichagua miguu ya Dele Alli kufanya kazi yake.

Alli ni mchezaji muhimu kwa Mourinho wa sasa, licha ya kipindi cha miezi 18 ya karibuni kusumbuliwa na majeraha, bado Dele amepewa namba za siri ‘password’ za kuwafungua wapinzani.

Mipango yote ya Tottenham ipo chini yake, ndiye anayeweza kuamua kubadili mwelekeo wa mpira wakati wa kushambulia, Eric Dier na Harry Winks wapo kama walinzi wa Alli, wanamlinda kwa kumkabia na kumpa mipira ambayo ataweza kuitasfiri na kupeleka balaa kwa wapinzani.

Michezo miwili ya kwanza imeonesha hilo, tayari mchezaji huyo raia wa England amefunga bao moja na kutoa asisti mbili. Anacheza huru nyuma ya mshambuliaji wa kati.

“Napenda namba 10 ambaye anafunga mabao, nampenda namba 10 anayeingia ndani ya boksi, kwa upande wangu namba 10 ni nane na nusu pindi timu inapopoteza mpira, pia, ni tisa na nusu pindi timu inapokuwa na mpira,” alisema Mourinho mwaka 2015, wakati ambao Tottenham walishinda mabao 5-3 dhidi ya Chelsea na Alli kuwa nyota wa mchezo huo.

Wakati anaingia kwa mara ya kwanza Chelsea, licha ya kuwa na kundi kubwa la wachezaji wenye uwezo na ubora mkubwa, Frank Lampard alikuwa kipenzi cha Mourinho, hakumpa kitambaa cha unahodha.

Ila, alikuwa mchezaji ambaye aliifanya kazi ya Mourinho kwa urahisi ya kutafsiri falsafa za Mreno huyo, msingi mkubwa wa alichokitaka Jose kilikuwa katika miguu na akili ya Lampard.

Alipoenda Inter Milan, stori ilikuwa ile ile kasoro mtu wa kuifanya kazi hiyo. Hapa alikutana na Wesley Sneijder, Mdachi aliyemweka Sir Alex Ferguson katika wimbi zito la mawazo, kwani wakati wote aliamini ni mchezaji wa Manchester United aliyekuwa na jezi ya Inter Milan.

Kama ilivyokuwa kwa Lampard, naye Sneijder alikuwa moyo na ubongo wa falsafa ya Mourinho pale Giuseppe Meazza au San Siro kama ulivyotambuliwa na wengi.

Bado haikutosha, alifungasha safari mpaka katika Jiji la Madrid, ndani ya timu iliyohitaji kuondoa jinamizi la kushinda mataji baada ya kipindi kirefu kupita licha ya usajili wa mastaa kutoka kwa wababe wengine wa soka la dunia.

Real Madrid iliyokuwa na Cristiano Ronaldo, Ricardo Kaka, Sergio Ramos, Karim Benzema, Gonzalo Higuain, Xabi Alonso, Luka Modric, Sami Khedira, Angel di Maria lakini katikati ya kundi hilo la wachezaji Mourinho aliiamini akili ya Mesut Ozil.

Ozil hakukimbia sana uwanjani kama wengine, lakini palipo pagumu alipalainisha, mawazo ya akili yake yalitafsiriwa kwa uharaka zaidi na ubongo wa mbele, ambao kitaalamu unaitwa ‘Cerebrum’.

Wapinzani wote walitulizwa na kufia hapo, walijikuta watumwa wa kufanya kila alichokitaka Ozil, hakuna aliyeshangaa walipokuwa wakikimbiza kufuata nyayo zake.

Anazielewa mno ‘frequency’ za mpira, anajua ni wakati gani anatakiwa kutoa pasi na wakati gani anatakiwa kukokota mpira.

Ni ngumu sana kucheza na Ozil aliye katika kilele cha ubora wake. Kama kuna mchezo ambao Real Madrid waliupoteza pindi Mesut yupo juu ya kilele chake labda dhidi ya Barcelona. Huko kwingine, bahati iliamua kupita mbali nao.

Aliporejea Chelsea kazi yake aliifanya Eden Hazard, hata alipoenda Manchester United hakuwa mjinga kumsajili Paul Pogba.

Alli anaweza kuwa Sneijder mpya, Deco mwingine, Ozil wa Tottenham au Lampard wa Mourinho ndani ya White Hart Lane. Kipi kingine anahitaji? Jose tayari alishamtaja Dele kama mmoja wa viungo bora wa dunia?

SHARE
Previous articleDrake amefulia au imekuwaje?
Next articleMTAIPENDA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here