SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

KAA mbali na Simon Msuva. Dogo anazidi kujiwekea rekodi ndani ya kikosi cha Yanga kupitia michuano mbalimbali. Kwa saa ndiye mchezaji kinara wa mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa ametupia nyavuni mabao 10.

Achana na hilo, Msuva ndiye mchezaji mwenye rekodi ya kuifungia Yanga mabao ya awali katika michuano Yanga iliyoshiriki akianzia na Ligi Kuu Bara msimu huu.

Itakumbukwa kuwa winga huyo alifunga bao la kwanza katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara wakati Yanga ilipopata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Maafande wa JKT Ruvu, Agosti mwaka jana.

Hakuishia hapo, Januari mwaka huu, Msuva akatua kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar na kufanya yake kwa kufunga bao la kwanza Yanga ilipovuna ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Jamhuri ya Pemba.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, winga huyo akafanya kilekile kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ngaya De Mbe kwa kufunga bao safi wakati Yanga ilipowaadhibu bila huruma wenyeji wao hao kutoka Visiwa vya Comoro mabao 5-1.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here