SHARE

NA WINFRIDA MTOI

KITENDO cha Mtibwa Sugar kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, imekuwa ni sherehe kila kona kuanzia wachezaji, viongozi mashabiki walioibua mijadala mbalimbali katika mitandao ya kijamii.

Mtibwa ilifanikiwa kutwaa kombe hilo kwa kuifunga Simba bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

 Furaha imekuwa ni kubwa hasa kwa mashabiki ambao ni wapinzani wa Simba, wakiungana na wale wa Mtibwa Sugar kufanya kusherehekea.

Kikosi hicho kimewasili jana jijini Dar es Salaam na kupokewa na wapenzi wa Mtibwa na kwenda hotelini kupumzika.

Wachezaji wa timu hiyo wametupia picha  walizopiga na kombe lao kila sehemu katika mitandao yao ya kijamii, wakiwashukuru mashabiki kwa sapoti waliyowapa tangu wameanza michuano hiyo.

Kati ya wachezaji   ambao picha na video zake zimesambaa zaidi ni kiungo wa  timu hiyo, Abdulharim Humud ‘Gaucho’, aliyetamba kuwa walitarajia ushindi huo kwani waliingia uwanjani kukamilisha ratiba.

Humud alisema  aliwaambia  watu tangu awali kuwa  lazima wachukue ubingwa huo kwa sababu mechi ngumu walikuwa wameimaliza dhidi ya Yanga waliyokutana nayo nusu fainali.

“Mimi nilizungumza vile kutokana na uzoefu wangu wa soka la Tanzania na wale wasioamini nadhani kombe wameliona linakwenda Morogoro sasa, tunamshukuru Mungu kwa hilo,” alisema Humud.

Kwa upande wake Kocha Mkuu Zuberi Katwila, alisema  walijipanga na wachezaji wake walizingatia nidhamu ya mchezo na kushirikiana uwanjani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here