SHARE

JUZI ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa Watanzania, ikishuhudiwa umati wa mashabiki wa mchezo wa masumbwi wakiujaza Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam kushuhudia pambamo la bondia
Mtanzania Hassan Mwakinyo, dhidi Arnel Tinampay.

Katika pambano hilo, Mtanzania huyo alishinda dhidi ya Mfilipino kwa kupata pointi 97-93, 98-92 na 96-96 na kuibua shangwe kwa umati uliofurika katika uwanja huo.

Walioshuhudia pambano hilo, walipata faida mbili ikiwamo ya kushuhudia Mtanzania huyo akipata ushindi, lakini pia hamasa iliyoonekana kabla na wakati wa pambano hilo.

Lilikuwa ni tukio lililovunja rekodi kwa miaka ya hivi karibuni, hasa kwa mchezo wa ngumi ambao kadri siku zinavyozidi kwenda ulikuwa unazidi kudorora.

Sisi Dimba kama wadau wa michezo, tunampongeza kwanza Mwakinyo kwa ushindi ule mgumu alioupata mbele ya halaiki ya mashabiki ya Watanzania, lakini pia kwa hatua yake kurudisha heshima ya mchezo wa masumbwi.

Kadhalika pongezi zinastahili kwenda serikalini ngazi mbalimbali kutokokana na kumuunga mkono bondia huyo na hatimaye kuwa naye katika kipindi cha pambano lenyewe.

Tunaamini, sasa Watanzania wameamka na kujua umuhimu wao wa kutoa hamasa katika michezo mingine zaidi ya soka, bila shaka litakapotokea pambano lolote au mchezo mwingine wataendelea kuunga mkono ili tuweze kupiga hatua katika maeneo mengine ya michezo yetu.

Kwetu sisi Dimba hatufarijiki na ushindi tu, lakini inatukumbusha ile hamasa ya miaka ya nyuma wakati huo Tanzania ikiwa na mabondia maarufu kama akina Emmanuel Mlundwa, Habib Kinyogoli, Stanley Mabesi, David Mwaba, Willy Isangula na wengine ambao enzi zao waliiletea sifa kubwa nchi yetu.

Shime Watanzania kama tulivyoonekana katika siku za hivi karibuni tukijazana uwanjani kushuhudia timu ya Taifa ya soka ya Wanawake Kilimanjaro Queens ikicheza michuano ya Cecafa na leo hii tunashuhudia pambano la Mwakinyo likipata umati wa mashabiki, basi tuendelee kuunga mkono michezo mingine ambayo itaweza kutusogeza mbele kutoka hapa tulipo.

Kila la heri Mwakinyo katika safari yake ya kutafuta Ufalme wa msumbwi kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here