SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

YAPOTEZEE kwa muda mabao ya Amissi Tambwe wa Yanga akiwa kama kinara kwa wachezaji wa kigeni, mgeukie beki kisiki wa Simba, Method Mwanjali, alichowafanya maproo wote wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwanjali ambaye amekuwa nguzo kubwa katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, amefanikiwa kucheza michezo mingi kuliko wachezaji wengine wa kigeni.

Mzimbabwe huyo katika michezo yote sita ya Kombe la Mapinduzi ikiwemo fainali dhidi ya Azam, alikuwa ametumika kwa dakika zote 90 za kila mtanange kama ilivyokuwa kwa ligi ya bara ambapo alishuka uwanjani  mara 18.

Mwanjali ambaye amekuwa mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, alitangazwa kama nyota wa mchezo mara mbili kwa mechi mbili tofauti, rekodi ambayo haijafikiwa na mchezaji yeyote wa kigeni anayecheza soka nchini kwa msimu huu.

Tofauti na ilivyo kwa wenzake, Janvier Bukungu, Laudit Mavugo wa Simba, Donald Ngoma, Tambwe wa Yanga ambao walikosekana katika michezo kadhaa ya michuano hiyo, huku Haruna Niyonzima akicheza mechi zote lakini akifanyiwa mabadiliko mara kadhaa tofauti na ilivyokuwa kwa Mwanjali.

Kwa upande wa Azam, wachezaji wao wa kigeni ambao wameonekana kudumu kwenye kikosi cha kwanza ni Stephano Kingue, Yakubu Mohamed, ambao wamecheza michezo yote visiwani humo, lakini hao wamecheza mechi tatu za duru la pili katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here