SHARE

JESSCA NANGAWE

KWA takribani wiki nzima kumekuwa na mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu nafasi ya msemaji wa Yanga inayoshikiliwa na Dismas Ten mashabiki wakitaka ifanyiwe mabadiliko haraka.

Dismas Ten ameangushiwa jumba bovu kwa madai viatu vya usemaji wa klabu hiyo vinampwaya kutokana na kushindwa kwake kufanya hamasa ya watu wajitokeze kwa wingi katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika baina ya Yanga na Towship Rollers ya Botswana uliopigwa Jumamosi iliyopita uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mashabiki hao wamelazimika kumtolea uvivu Ten kutokana na Idara anayoiongoza ndiyo yenye jukumu la kuitangaza Yanga kila pembe ya dunia kama vile anavyofanya msemaji wa mahasimu wao jadi kisoka Haji Manara.

Mitazamo ya mashabiki wengi inamuona Dismas Ten siyo mtu sahihi anayeweza kuitangaza Yanga kwa upana wake lakini pia kushindwa kwake kumdhibiti Haji Manara ambaye amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuwapiga vijembe na kufanyia dhihaka mbalimbali mambo ambayo yamekuwa yakiwaumiza.

Kuyumba Ten kumewafanya mashabiki wa Yanga kumkumbuka aliyewahi kuwa msemaji wao Jerry Muro ambaye kwa namna fulani alionyesha kujaribu kuzima tambo za Manara na sasa wameanza kupendekeza majina ya watu wanaoona wanafaaa kuwa wasemaji wa klabu hiyo.

Miongoni mwa majina hayo wamo watangazaji wa kituo cha Redio Clouds Mbwiga wa Mbwiguke na Antonio Nigaz.Wengine ni chipukizi Ally Kamwe, Hassan Bumbuli, Masau Bwire na Athanas Kazighe ambao ni moja ya mashabiki wa Yanga wenye taaluma ya Uandishi wa Habari.

Kwa mtazamo wako kupitia orodha hiyo unadhani nani anafaa kuwa msemaji mpya wa Yanga baada Disman Ten kuonyeshwa mlango wa kutokea na uongozi wa klabu hiyo.

Tuma maoni yako kwenda namba 0717- 227681

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here