SHARE

TURIN, Italia

DUNIA haina siri, taarifa zinadai kuwa kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ameshafanya mazungumzo ya kujiunga na Juventus msimu ujao.

Imebainika kuwa Juventus hawaridhishwi na Maurizio Sarri aliyerithi mikoba ya  Massimiliano Allegri ambaye alishinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu ya Italia, Scudeto akiwa kocha hiyo.

Juventus wanaamini Guardiola ni mtu sahihi wa kukiongoza kikosi chao kilichosheheni mastaa wengi, pia, inaelezwa wanamuhitaji kocha huyo kwa ajili ya kutanua soko lao kibiashara kama walivyofanikiwa kwa staa wao Cristiano Ronaldo.

Hata hivyo, Guardiola alikana tetesi hizo kwa kusema kuwa bado ana kazi kubwa ya kuifanya ndani ya kikosi hicho cha Manchester City ambayo inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England.

Guardiola alidai taarifa hizo hazina ukweli wowote sababu bado ana mkataba wa kuitumikia Manchester City lakini imebainika kuwa huu  ni msimu wa mwisho wa kocha huyo ndani ya kikosi hicho.

Kocha huyo raia wa Hispania amefanikiwa kutwaa mataji zaidi ya matatu ndani ya kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Manchester ambayo ni Ligi Kuu (2), Kombe la Carabao (2), Kombe la FA na Ngao ya Jamii.

Pia, taarifa zilizopo zinadai mabingwa hao wa Ligi Kuu Italia, Seria A mara nane mfululizo wapo kwenye mpango wa kumshawishi mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi kujiunga na kikosi chao.

Itakumbukwa msimu uliopita, wababe hao wa Seria A walimsajili Ronaldo kutoka Real Madrid, safari hii wamedhamiria kuwaunganisha wawili hao katika kikosi kimoja sababu Messi hajawahi kucheza timu nyingine zaidi ya Barcelona.

Hivi karibuni, ndani ya kikosi cha Barcelona kumekuwa na sintofahamu ambazo zimesababisha baadhi ya wachezaji akiwamo Messi kumtolea maneno makali Mkurugenzi wa Ufundi, Eric Abidal.

Pia, taarifa zinaeleza Messi ambaye amekuwa akikitumia kikosi hicho kwa zaidi ya miaka 10, anashawishika kuondoka mwishoni mwa msimu huu kutafuta changamoto nyingine nje ya Barcelona.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here