SHARE

 

LONDON, England

MLINZI wa kati wa klabu ya Arsenal, Gabriel Paulista, ameibuka na kuwatuliza presha mashabiki wa klabu hiyo kwa kuweka wazi kuwa yupo fiti na majeraha yake si makubwa sana.

Mbrazil huyo alitolewa nje kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Manchester City, baada ya kuumia enka katika mchezo huo uliopigwa wikiendi iliyopita ambapo vijana hao wa Emirates waliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Washika mitutu hao wa London watamkosa beki Per Mertesacker ambaye atakaa nje ya uwanja hadi katikati ya Desemba kutokana na maumivu ya goti na kocha wa klabu hiyo, Arsene Wenger, alikiri kuwa anahitaji kusajili beki mwingine.

Hata hivyo, picha iliyotumwa kwenye akaunti rasmi ya mtandao wa Instagram ikimuonesha Paulista akifanya mazoezi ilionesha wazi kuwa beki huyo huenda akarudi kweli baada ya muda mfupi.

Picha hiyo ilisindikizwa na maneno haya: “Leo (jana) najisikia vizuri, si tatizo kubwa. Nawashukuru mashabiki wangu kwa salamu za pole.”

Hivi karibuni klabu ya Arsenal ilihusishwa kuwataka walinzi wawili wa kati, Jonny Evans (West Brom) na Shkodran Mustafi wa Valencia, ambapo mmoja kati ya hao anaweza kutua Emirates.

Aidha, kutokana na beki kisiki Laurent Koscielny kuwa kwenye mapumziko ya muda mrefu, Wenger anategemewa kuwaanzisha mabeki Calum Chambers na Rob Holding katika kikosi cha kwanza dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England.

Lakini Mfaransa huyo hatakuwa na matumaini ya kuwategemea zaidi mabeki hao wasio na uzoefu katika michezo migumu ikiwemo dhidi ya Leicester na Chelsea ndani ya mechi sita za awali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here