SHARE

LONDON, England


 

MKONGWE wa zamani wa klabu ya Arsenal, Emanuel Petit, amesema anaamini kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, atafanikiwa kutinga fainali ya Europa League licha ya kuandamwa na mzimu wa kupoteza fainali tatu za Ulaya.

Katika miaka 22 ya Wenger akiwa Arsenal, kocha huyo alishindwa kunyakua taji la Washindi wa Ulaya mwaka 1992 dhidi ya Monaco, pia akibamizwa kwenye fainali ya taji la UEFA mwaka 2000 na Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006 dhidi ya Barcelona.

Hata hivyo, kocha huyo amefanikiwa kuifikisha Arsenal kwenye hatua ya nusu fainali Europa League, akikabiliwa na mtihani wa kuiondoa Atletico Madrid katika mchezo wa marudiano utakaochezwa kesho kwenye dimba la Wanda Metropolitano.

Mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Emirates baina ya timu hizo, Atletico iliilazimisha Arsenal sare ya bao 1-1 na kuwaweka washika mitutu hao wa London kwenye wakati mgumu wa kutinga fainali itakayochezwa Mei 22, mwaka huu, jijini Lyon, Ufaransa.

Licha ya Arsenal kukabiliwa na jukumu hilo, Petit anaamini Wenger atapata bahati ya kuiondoa Atletico kesho na kucheza fainali.

“Itakuwa ni jambo zuri kwa Wenger kuingia fainali dhidi ya Marseille,” alisema Petit.

“Marseille tayari wameshaingiza mguu mmoja kwenye fainali (baada ya kuifunga Red Bull Salzburg mabao 2-0 kwenye nusu fainali nyingine iliyochezwa wiki iliyopita).

“Itakuwa ni hadithi tofauti kwenye mechi yao ya marudiano dhidi ya Atletico ila kuna sababu nyingi zinazoniaminisha Wenger ana nafasi ya kusonga mbele,” aliongeza.

“Nina matumaini ana uwezo wa kufika fainali na kunyakua taji kwa sababu anastahili, lakini kama hatofanikiwa natumai pia mashabiki watampa heshima yake. Anachokihitaji kwa sasa ni wachezaji wake wawe fiti asilimia 100 kiakili na kimwili hasa wanapokutana na straika kama Diego Costa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here