SHARE

EZEKIEL TENDWA NA SAADA SALIM

MASHABIKI wa Simba wanatamani sana kumwona mshambuliaji, Laudit Mavugo baada ya kutajwa sana lakini wakisikia habari hii wataelewa kwanini straika huyo mwenye uwezo wa kupachika mabao amechelewa kuwasili kujiunga na wenzake.

Ishu iko hivi; Simba wameweka wazi kwamba wamemalizana na mshambuliaji huyo zamani sana na kinachomzuia kutua nchini ni kutokana na kushiriki michuano ya Rais Cup, inayodhaminiwa na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.

Kigogo mmoja wa Simba ameliambia DIMBA Jumatano kuwa michuano hiyo ndiyo inayosababisha straika huyo kushindwa kuwasili nchini mapema lakini baada ya kumalizika kwa michuano hiyo atawasili.

“Mavugo tulifanya naye mazungumzo tangu mwaka jana na sasa tunamalizia tu mambo machache ila kinachomchelewesha ni kutokana na michuano ambayo wenyewe wanaiita ‘Rais Cup’.

“Nasikia michuano hiyo inadhaminiwa na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza. Tumemuacha amalizie michuano hiyo ndipo atakuja, hizo taarifa zilizopo kwamba Vital’O wamemwongezea mkataba hazina ukweli wowote,” alisema.

DIMBA Jumatano lilifanya mawasiliano na Mavugo ambaye alisema kuna majukumu yaliyombana ndiyo maana anachelewa kuja nchini, lakini akiyamaliza tu anatua kuungana na wenzake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here