SHARE

MANCHESTER, England

NYOTA wa Manchester United, Marcus Rashford kwa sasa anaishi katika ndoto zake katika maisha yake ya soka ndani ya miamba hiyo ya Old Trafford.

Katika umri wa miaka 22, amecheza michezo zaidi ya 200 akiwa na mabingwa hao wa zamani wa England, amefunga mabao 64 na kufanikiwa kushinda mataji matatu, pia, ameiwakilisha England mara 38.

Rashford tayari ni mmoja wa wachezaji wa Manchester United wanaoingiza mkwanja mrefu kwa wiki, analipwa pauni 250,000 na marupurupu mengine, huku akivaa jezi namba 10 ambayo iliwahi kuvaliwa na wachezaji kama Wayne Rooney, Ruud van Nistelrooy, Teddy Sheringhan na David Beckham.

Pamoja na yote hayo, bado anashindwa kuisaidia klabu yake kwa kucheza kwa ubora wake kila timu hiyo inapokuwa uwanjani, isipokuwa amekuwa mchezaji wa vipindi. 

Bado ana safari ndefu ya kuirudisha United kwenye makali yake kama moja ya klabu bora barani Ulaya na Ligi Kuu England. Ni kweli alikuwa na uwezo huo unaotajwa na mashabiki wa Manchester United?

Rashford alianza kupata nafasi kikosi cha kwanza akiwa na umri wa miaka 18, mchezo wa kwanza alicheza dhidi ya Midtjylland FC na kufunga mabao mawili. Aliendelea kwa kupachika idadi kama hiyo ya mabao dhidi ya Arsenal katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England.

Msimu huo, alifunga bao pekee lililoipa ushindi Manchester United dhidi ya majirani zao Manchester City na Aston Villa, pia, ilimchukua dakika tatu tu kufunga bao lake la kwanza akiwa na jezi ya England.

Sasa ukiangalia nyuma, wakati huu ambao Manchester United wanahitaji mchezaji ambaye ataifikisha klabu hiyo katika ndoto zao, Rashford hajawa kwenye mwendelezo wa kiwango mzuri kama ilivyokuwa miezi minne ya kwanza wakati ule.

Ilionekana muda bado, lakini hajabadilika kwa muda mrefu na haonekani kupiga hatua kwenda mbele katika maendeleo binafsi uwanjani na timu kwa ujumla.

Ni vibaya kusema hajafanya mambo mazuri ndani kikosi hicho tangu apate nafasi. Lakini zipo ngapi, zinahesabika kwa urahisi hata kwa vidole kwa mkono mmoja.

Takwimu za ufungaji mabao za Rashford hazijawahi kuwa nzuri tangu apate nafasi katika kikosi cha kwanza. Alifunga mabao 8 katika michezo 18 msimu wa 2015/16. Rekodi zake nzuri zilikuwa msimu uliopita alipofunga mabao 10 kwenye mechi 33 za Ligi Kuu, na mabao 13 ndani ya mechi 47 za michuano yote alizocheza msimu uliopita.

Kwa mshambuliaji anayecheza michezo mingi, mashabiki wa Manchester United ilibidi watarajie zaidi ya hicho, yaani mabao 15, 20 ikiwezekana 25 kwa msimu.

Kuliweka jambo hilo kwa ufafanuzi zaidi, straika wa Chelsea, Tammy Abraham, ana miaka 21 kama Rashford, ameshafunga mabao saba ya Ligi Kuu England, amebakiza mabao matatu tu kufikia msimu bora wa nyota huyo wa Manchester United.

Rashford kwa wakati wote atacheza ndani ya kikosi cha Manchester United, ingawa, kwa upande mwingine, majeraha yanatajwa kurudisha kiwango chake nyuma, sababu alianza kutegemewa akiwa na umri wa miaka 18 tu.

Kabla, alikuwa akiongozwa na Zlatan Ibrahimovic, Romelu Lukaku na Alexis Sanchez, alitumika kama straika wa pili au mbinu mbadala nyuma ya hao wengine. Sasa ni mchezaji ambaye anaangaliwa na timu nzima pale mbele, bado mchezaji huyo anayevalia jezi namba 10 ameshindwa kufanya vizuri. 

Hawezi kuwa Kylian Mbappe, ambaye ameonyesha uwezo mkubwa kila alipohitajika ndani ya klabu yake na taifa lake. Rashford kwa miaka minne ya karibuni hajafika levo za Mfaransa huyo.

Ni ngumu kwa straika mdogo kufanya mambo makubwa na kufunga mabao pindi wanapopata nafasi kwa mara ya kwanza kikosini, kwa Manchester United hilo limekuwa la kawaida, tulishawaona akina Federico Macheda, Danny Welbeck na James Wilson ndani ya miaka 10 iliyopita, lakini wote walishindwa kufika katika kilele cha mafanikio.

Rashford ana mbinu za kuweza kufanikiwa, lakini kama akifanya maamuzi na kuwa kwenye mwendelezo ndani ya Ligi Kuu, hicho ndicho anachokosa straika huyo raia wa England.

Anatakiwa kujua wapi anatakiwa kuwa kwa wakati sahihi, wakati gani wa kutoa pasi, muda gani wa kukimbia, wapi kwa kupiga kisigino au kufanya mambo mengine, akifanikiwa kuyajua hayo atakuwa mmoja wa straika hatari.

Mwangalie Rashford akicheza, si muda wote anaweza kukufurahisha. Wakati mwingine, anashindwa kufanya mambo kwa urahisi, anajipa wakati mgumu mwenyewe, anahitaji msingi mzuri.

Katika umri wa miaka 21, Cristiano Ronaldo alionekana akijifunza zaidi, alikuwa kama mtu anafanya jukumu la kutafsiri kile alichokiona mazoezini uwanjani, alifanikiwa na kila kitu kilienda kwenye njia sahihi kwa upande wake.

Rashford hawezi kufanana na Ronaldo kiuchezaji na uwezo, lakini wanaelekeana kwa upande mmoja, anatakiwa kujifunza na kuwa mwelewa zaidi, kwa wachezaji wadogo wenye vipaji huwa ngumu kufika kwenye mafanikio. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here