SHARE

KAZI sasa inatarajiwa kwa timu zinazoshiriki michuano ya ligi kuu, hii ni baada ya maboresho ya ratiba yaliyofanywa hivi karibuni.
Baada ya mabadiliko hayo, mechi kadhaa zitachezwa Jumamosi na Jumapili ijayo, ambapo Simba itacheza na Azam FC ikiwa ni moja ya mechi kubwa za mwanzoni tangu kuanza kwa michuano hiyo Agosti 26.
Siku hiyo pia kutakuwa na mechi itakayoikutanisha Tanzania Prisons dhidi ya Majimaji.
Siku ya pili Septemba 10, Njombe Mji itacheza na Yanga mjini Njombe, Mtibwa Sugar itaumana na Mwadui, Lipuli itacheza mechi yake ya pili dhidi ya Stand United, wakati mechi nyingine mbili zitahusisha timu ya Singida United itakayocheza na Mbao FC, wakati Mbeya City ikijipima ubavu na Ndanda FC.
Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi, ratiba hiyo sasa itakwenda vizuri na itakuwa ikisimama pale tu ambapo kutakuwa na michezo iliyomo katika kalenda ya Fifa.
Sisi Dimba kwanza tunarudia tena kupongeza hatua ya TFF kuifumua ratiba ile ya awali na kuipanga upya kwa kuzingatia mahitaji ya kalenda, tunaamini hili litaondoa mizengwe na ubabaishaji.
Hata hivyo, tunafahamu licha ya nia hiyo nzuri ya TFF, bado zipo klabu zilizokuwa na mazoea ya kutoa visingizio mbalimbali hasa pale inapotokea timu zao zinafanya vibaya.
Haya yasipewe nafasi, Dimba tunajua kwamba kulegalega kwa maamuzi kutoka TFF kuliharibu mambo mengi katika soka la Tanzania, ambapo sasa tunapata matumaini mapya ya kufufua maendeleo ya mchezo wa kandanda hapa nchini.
Sisi Dimba tunaamini kuwa michuano ya mwaka huu itakuwa ya wazi na italeta bingwa anayestahili kwa kufanya vizuri uwanjani.
Kwetu hatuoni hata dalili ya ubabaishaji hasa gonjwa sugu la kuahirisha mechi za ligi ambalo kwa muda mrefu kupitia maoni yetu tumelikemea bila mafanikio.
Ni imani yetu kwa sasa kwamba, klabu zitajikita katika ushiriki wa michuano hiyo bila ya wasiwasi maana kama litaweza kutibika tatizo hili sugu, haya mengine kama vile ya waamuzi tunadhani hayawezi kuwa na changamoto tena.
Tunazitakia heri na mafanikio timu zote zinazoshiriki ligi kuu msimu huu, tunaamini mafanikio watakayoyapata yatalisogeza mbele soka letu na hata kutupatia timu bora ya Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here