SHARE

NA JESSCA NANGAWE

PANGA la Yanga tayari limepita huku kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Bernard Morrison, akiendelea kusalia ndani ya kikosi hicho msimu ujao.

Yanga imewakata takribani wachezaji 14 huku wengine 17 wakisalia sambamba na jina la kiungo huyo ambaye licha ya kukumbwa na matukio mengi ya utovu wa nidhamu, jina lake lipo kwenye orodha ya majembe yalisosalia Jangwani.

Morrison ambaye uwanjani anaaminika kuwa bora, amejikuta akiwagawa mashabiki wa timu hiyo wengi wakiridhia aondolewe kutokana na kufanya matukio mfululizo ambayo yanatajwa kuigharimu timu.

Pamoja na mwenyewe kuchanganya habari kuhusu mkataba wake akidai tayari ulimalizika tangu mwezi uliopita, viongozi wa timu hiyo waliendelea kusisitiza winga huyo ana mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuitumikia Yanga.

Zifuatazo ni sababu tatu ambazo DIMBA Jumatano zimeainisha zilizomunusuru raia huyo wa Ghana kubaki licha ya vitimbi vyake.

 

UWEZO BINAFSI

Pamoja na visa vyote anavyofanya, ukweli ni kwamba Morrison bado ni mchezaji mzuri na mwenye msaada mkubwa kwa timu katika kujenga mashambulizi na hata upachikaji mabao.

Mchezaji huyo pia ni mahiri katika upigaji wa mipira ya adhabu, ushahidi ni lile bao lililompaisha alilowafunga watani wao wa jadi Simba, wakipata ushindi wa bao 1-0.

 

TISHIO LA KWENDA SIMBA

Katika kile kinachoonekana kuwawekea ngumu Simba, Yanga ilibidi kumbakiza kikosini Morrison, hii inatokana na siku za hivi karibuni, winga huyo kuhusishwa na tetesi za kusaini mkataba na watani wao wa jadi Simba.

Licha ya Simba kukataa mara kadha kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Senzo Mbatha, timu hizi mbili huwa haziaminiani hususna katika masuala ya usajili.

 

GHARAMA ZA KUVUNJA MKATABA

Kwa kipindi chote, Yanga imekuwa ikidai kuwa na mkataba wa miaka miwili na winga huyo licha ya mwenyewe kukana, hivyo suala la kumwacha mchezaji huyo na endapo Yanga ingekuwa kweli ina mkataba basi wangelazimika kutoa kitita kirefu cha fedha kwa ajili ya kiuvunja mkataba huo.

 

Mkurugenzi wa kampuni ya GSM, Hersi Saidi, ambao ndiyo wanaosimamia usajili kipindi hiki, alisema Morrison bado ni mchezaji wao halali na kuhusu masuala yake ya utovu wa nidhamu uongozi utashughulikia na kuyaweka sawa.

Hata hivyo kumekuwa na taarifa kwamba kiungo huyo anatakiwa na klabu moja nchini Kuwait pamoja na nyingine ya Afrika Kusini, pia ikidaiwa amekuwa akiwindwa na mahasimu wao Simba ambao wanataka kuongeze nguvu msimu ujao licha ya kutotaka kuzungumzia hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here