SHARE

NA WINFRIDA MTOI

KUMEKUWA na tetesi kuwa straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi, anataka kurejea katika kikosi hicho msimu ujao.

Okwi aliondoka Simba msimu uliopita baada ya mkataba wake kumalizika na kupata dili la kujiunga na Al Ittihad ya Mirsi iliyomuona wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON).

Mchezaji huyo kipenzi cha Wanasimba, aliondoka kipindi ambacho alikuwa bado anahitajika Msimbazi, hivyo ikawalazimu kumsajili Mbrazil, Wilker da Silva, kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji lakini alishindwa kuonyesha makali.

Okwi ni mchezaji aliyekuwa na msaada mkubwa wakati Simba ilipotinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo kuondoka kwake ikawa ni pengo.

Imekuwa ni kawaida kwa nyota huyo Mganda kuondoka Simba na kurejea tena, ameshafanya hivyo mara tatu.

Katika kipindi hiki, tetesi zinasema mchezaji huyo yuko mbioni kurejea tena Msimbazi, ukizingatia pengo lake bado halijazibwa.

Kingine kinachoonekana Okwi anahitajika kurejea katika timu hiyo, ni maandalizi ya Simba kuelekea kwenye mchuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa sababu nafasi ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni kubwa.

Ikumbukwe Okwi alijiunga na Simba kwa mara ya kwanza mwaka 2010 akitokea SC Villa ya Uganda, akacheza hadi 2013, akauzwa kwenda Étoile du Sahel ya Tunisia.

Hata hivyo alikaa kwa muda mfupi katika timu hiyo ambayo iliamua kumtoa kwa mkopo SC Villa ambapo hakudumu na kurejea Tanzania kujiunga na Yanga katika msimu wa 2013/14

Alicheza Yanga kwa muda mfupi, kisha kurejea Simba ambapo alicheza kwa mwaka mmoja kabla ya kutimkia Sonderjyske ya Denmark aliyocheza kuanzia mwaka 2015 hadi 2017.

Baada ya kumaliza mkataba, Okwi alimua kurudi tena katika timu yake ya zamani, SC Villa lakini hakudumu akarudi Simba msimu wa 2017/18.

Kulingana na mtindo huo wa Okwi wa kwenda na kurudi Simba, timu ambayo inamfanya ang’are na kuzivutia klabu nyingine, itakuwa ni sababu ya mchezaji huyo kutajwa kurejea Msimbazi.

Hata Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Usajili ya Klabu hiyo, Zakaria Hanspope, aliwahi kusema kuwa, Simba ndiyo sehemu inayomfanya Okwi, ang’are siku zote.

Alisema kutokana na hilo, inamfanya mchezaji huyo kuondoka na kurudi, imekuwa ni jambo la kawaida kwake na Wanasimba wanamchukulia kama mtoto wao, wanampokea muda wowote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here