SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

PAZIA la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, inatarajiwa kufunguliwa leo huku wenyeji Serengeti Boys wakipepetana na Nigeria kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam huku mawazo yakiwa kusaka tiketi ya Kombe la Dunia kwa vijana nchini Brazil.

Mchezo huo wa ufunguzi wa michuano hiyo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika nchini, unatarajiwa kupigwa kuanzia saa 10:00 jioni, ukitanguliwa na mchezo kati ya Uganda na Angola kuanzia saa 8:00 mchana.

Serengeti Boys wanashuka uwanjani wakiwa na morali ya kutoka kufanya vizuri katika michuano ya maandalizi waliyoalikwa nchini Rwanda, ikijivunia kuichapa Cameroon ambayo ni moja ya timu zinazoshiriki Afcon.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Oscar Milambo, alisema maandalizi waliyoyafanya ni mazuri na wanatarajia kupata matokeo mazuri na kutwaa ubingwa huo.

 “Maandalizi tuliyoyafanya ni mazuri. Ninatarajia kwamba vijana wangu watafuata maelekezo tuliyowapa na kuibuka na ushindi mchezo huo wa ufunguzi.

“Malengo yetu ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa huo ikizingatiwa kuwa sisi ndio wenyeji. Najua kwamba ni kazi ngumu lakini maandalizi mazuri yananipa jeuri kuwa ushindi utapatikana,” alisema.

Kocha huyo amewaomba Watanzania wote kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa sapoti vijana wao kama walivyofanya kwa Taifa Stars hasa ilipocheza dhidi ya Uganda.

“Katika mchezo ule dhidi ya Uganda, Watanzania walijitokeza kwa wingi sana na hilo liliwapa morali wachezaji. Nawaomba wafanye hivyo tena pale Serengeti Boys itakapokuwa inacheza,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here