SHARE

JANA Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya uchaguzi na kupata viongozi wapya, ambao ni Rais, Makamu wa Rais na wajumbe wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo. Uchaguzi huo ulifanyika mjini Dodoma, baada ya uongozi wa Jamal Malinzi kufikia tamati, ukidumu kwa miaka minne.

Kuchaguliwa kwa viongozi hao ni ishara kwamba kuna jambo ambalo wapiga kura wameliona kuwa linaweza kufanywa na viongozi hao wapya, ambao wamechaguliwa jana na wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF.

Kimsingi ni kwamba, uchaguzi wa TFF umekwisha na hivi sasa Watanzania wanahichokitaka ni maendeleo ya soka, lakini pia utekelezaji wa yale ambayo viongozi hawa waliyaahidi kwa wapiga kura.

Ningependa kukumbusha kidogo tu baadhi ya mambo muhimu ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele na wadau wa soka kwa miaka mingi na hayajaweza kushughulikiwa kwa kiwango kilichotakiwa kama ambavyo wengi wanayatarajia kuyaona yakishughulikiwa na mamlaka husika.

Moja ya mambo makubwa kwenye soka la Tanzania ni maamuzi, hasa kwenye Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza pamoja na michuano mingine mbalimbali inayosimamia na TFF au vyama vya mikoa, jambo ambalo limekuwa likileta vurugu pamoja na matatizo makubwa kwenye viwanja mbalimbali hapa Tanzania.

Marefa wengi wa Tanzania wamekuwa kikwazo kwa baadhi ya timu kushindwa kupata matokeo bora, waamuzi wamekuwa kiini cha malalamiko na vurugu uwanjani kwa sababu hawatendi haki kama ambavyo inatakiwa.

Utendaji huo mbaya wa haki mara nyingi unaendana na kutafasiri na kuzisimamia sheria 17 zinazoongoza soka na hilo ndilo linalosababisha kuwapo kwa matatizo kwenye ligi yetu na kuifanya isipate bingwa sahihi, hivyo kuwa na bingwa ambaye hawezi kuwa na ushiriki bora katika michuano ya kimataifa.

Jambo jingine ni kuimarisha timu za taifa ambazo kwenye soka la Afrika na dunia tumekuwa hatufanyi vizuri kama nchi. Hili ni tatizo kubwa ambalo kama nchi, lazima tuliangalie vyema, kwa sababu ndio utambulisho wetu.

Hata kama tungekuwa na ligi bora kwa kiwango gani, lakini suala la timu imara ya taifa ni kitu muhimu zaidi, kwani ndiyo inaweza kuwa heshima kwa nchi kutokana na ukweli kwamba ni kilelezo cha soka letu.

Kwa maana hiyo, viongozi wapya wanatakiwa kuhakikisha kwamba nchi inapiga hatua katika soka, hasa kwenye soka la kimataifa, kwani hatuko vizuri. Tumeshindwa kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa miaka 30 sasa, hivyo hatua madhubuti na makusudi zichukuliwe ili kuleta heshima kwa nchi.

Mwisho ni kukomesha vitendo vya rushwa kwenye viwanja mbalimbali, ambapo suala la hili limekuwa sugu kwa miaka mingi. Tumesikia malalamiko ya makocha na hata wachezaji wamekuwa wakieleza kuwa kuna vitendo vya rushwa na kusababisha upangaji wa matokeo.

Hili linasababisha matatizo makubwa kwenye soka letu, kutokana na ukweli kwamba kuna baadhi ya timu zimekuwa zikipanga matokeo kutokana na rushwa au waamuzi kutoa maamuzi ya hovyo kwa kuwa wamepewa rushwa.

Ndiyo maana nasisitiza kwamba, ligi ya mwaka huu imefika ikiwa chini ya uongozi mpya wa TFF, hivyo ni lazima waangalie mambo yanayolalamikiwa na kupigiwa kelele ili kupata ligi bora yenye kuleta matokeo bora ambayo itasaidia kupata timu bora ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here